January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dar yaibuka kidedea UMISSETA Taifa

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, TABORA

MASHINDANO ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Tabora kuanzia Juni 16 hadi Juni 25 mwaka huu yamefikia tamati leo huku Mkoa wa DSM ukiibuka mshindi wa jumla katika Mikoa yote 31 ya Bara na Visiwani.

Akihitimisha mashindano hayo katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Deogratias Ndejembi amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu michezo kuendelea kufanyika katika ngazi zote ikiwemo shule za msingi na sekondari.

Amesema mashindano hayo ni muhimu sana kwa kuwa yanasaidia kuibua vipaji vya watoto katika fani mbalimbali, kuchochea uchumi wa wananchi katika Mkoa husika, kuboreshwa kwa miundombinu ya michezo katika shule za Mkoa husika na kujenga mahusiano na ushirikiano mzuri wa walimu na viongozi mbalimbali wa sekta ya michezo.

Mbali na Mkoa wa DSM kuibuka bingwa wa jumla katika michuano hiyo, Mikoa iliyoibuka kidedea kwa ushindi wa jumla katika mchezo mmoja mmoja ni kama ifuatavyo.

Soka la wanawake bingwa ni Dodoma akifuatiwa na Tabora na Manyara na Soka la wanaume bingwa ni Geita akifuatiwa na Mbeya na Rukwa.

Katika Mchezo wa riadha kwa wanawake bingwa ni Mkoa wa Pwani ukifuatiwa na Tabora na Arusha na kwa upande wa wanaume bingwa ni Mkoa wa Mara ukifuatiwa na Manyara na Pwani.

Upande wa Sanaa za ndani bingwa wa jumla ni Mkoa wa Tanga ukifuatiwa na DSM na Mtwara.

Aidha katika suala la usafi Mkoa wa Mara umeongoza kwa upande wa wasichana ukifuatiwa na Tanga na Njombe na kwa upande wa wavulana Mkoa wa Dodoma umeongoza ukifuatiwa na Tabora na Kilimanjaro.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Deogratias Ndejembi akihutubia umati wa wana michezo, viongozi na wakazi wa Mkoa wa Tabora katika kilele cha mashindano ya UMISSETA Taifa yaliyomalizika leo Mkoani hapa.
Wanafunzi wanamichezo kutoka Mkoa wa DSM wakishangilia ushindi wa jumla wa Michezo ya UMISSETA mwaka huu Mkoani Tabora.