Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online ARUSHA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wazazi, walezi pamoja na jamii kuwajibika katika kufuatilia mienendo ya watoto ili kubaini mabadiliko hasi ya kitabia yanapojitokeza.
Rais Samia amesema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Aidha, Rais Samia amesema kutowajibika kwa wazazi husababisha watoto kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya hivyo ni vyema kuwalinda watoto dhidi ya dawa hizo pamoja na vitendo vingine vilivyo kinyume na mila, desturi, maadili na silka zetu.
Rais Samia pia ameitaka jamii kuimarisha ushirikiano na viongozi wa dini pamoja na viongozi wa kijamii wakiwemo machifu kwa kuwa ndio walinzi wakuu wa maadili, utamaduni, mila na desturi.
Vile vile, Rais Samia amesema tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini na duniani kwa ujumla limekuwa likiongezeka na madhara yake ni makubwa na wakati mwingine athari zake ni za kudumu kwa jamii.
Hali kadhalika, Rais Samia amesema mbali na kupoteza nguvu kazi ya uzalishaji, matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa kichocheo cha vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi na unyang’anyi na hata kuambukizana maradhi kama UKIMWI na TB.
Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kutoka nchi zinazozalisha kwa zaidi ya asilimia 90.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa