November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini watoa tamko uwekezaji wa DP World bandari ya Dar-es-Salaam

 

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

Baadhi ya viongozi wa dini mkoani Mwanza,wamewataka  viongozi wenzao wa dini pamoja na wanasiasa nchini kutoliingiza taifa kwenye mtafaruku wa kuligawa taifa kwa sura ya ukabila,udini wala ukanda kuhusiana na uwekezaji wa uendeshaji wa bandari .

Pia wameshauri serikali na watalaamu wabobezi wa sheria katika masuala ya mikataba waendelee kuwaelimisha Watanzania kuhusu uwekezaji huo na wananchi wajadili kwa heshima na staha jambo hilo wakitambua tayari limepitishwa Bungeni.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza, wakimsikiliza Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo Sheikhe Hasani Kabeke (wa pili kutoka kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wa habari (hawapo pichani) jijini humo baada ya viongozi hao kutoa tamko

Hayo yamebainishwa wakati wakitoa  tamko hilo nyakati tofauti  jijini hapa na Wenyeviti Wenza wa Kamati ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza,Askofu Charles Sekelwa na Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke.

Askofu Sekelwa amesema katika ziara iliofanywa na Rais Dk.Samia alikutana na viongozi wa dini,akatumia fursa hiyo kuzungumza na kutoa ufafanuzi yeye mwenyewe kuhusu mkataba wa uwekezaji wa DP World baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai,kwa hakika viongozi hao walimwelewa na kumpongeza kwa jitihada na hatua anazoendelea nazo za kuliletea taifa maendeleo taifa.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, Dk. Askofu Charles Sekelwa (kushoto) akisoma tamko la viongozi wao kuhusu mkataba wa DP World wa uwekezaji wa bandari,wa pili kulia Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke.

“Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, imekuwa na ada ya kukutana kila baada ya miezi mine kujadili kazi za kamati na mambo mbalimbali ya mustakabali wa nchi yetu,mkutano wetu wa leo pamoja na mambo mengine tumepitia na kujadili ziara ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aliyoifanya mkoani Mwanza kuanzia Juni 13 hadi 14,2023,ziara ambayo imeleta matumaini makubwa kwa wana Mwanza na Kanda ya Ziwa,” amesema Dk.Askofu Sekelwa.

Pia Askofu  Sekelwa amesema serikali na wanasheria wasomi waliobobea katika tasnia hiyo waendelee kuwaelimisha Watanzania uwekezaji huo huku upande wa wananchi wakiendelea kujadili jambo hilo kwa heshima na staha wakitambua kuwa Bunge limeshalipitisha kwa niaba yao baada ya kujadili na kutoa maoni yao ya namna ya kuboresha kwa maslahi ya Watanzania.  

“Chonde chonde tunawaomba wanasiasa, viongozi wenzetu wa dini na watu wote wenye mapenzi mema na nchi yetu,wasiilingize na kulijadili jambo hili kwa sura ya ukabila, udini wala ukanda,wajadili kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa letu, muhimu wafahamu na kukumbuka kuwa uwekezaji huo nchini Tanzania si wa kwanza kufanyika,kwa nyakati na tawala tofauti umekuwepo uwekezaji maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu,”amesema kiongozi huyo wa kiroho.

Pia katika mkutano wao huo na Rais Dk. Samia walipata kufahamu kuwa DP World hawajawekeza Tanzania pekee bali wamewekeza barani Afrika katika nchi za Algeria,Angola,Afrika Kusini,Djibout,Misri,Msumbiji,Nigera, Rwanda,Senegal na Somaliland na baadhi ya mataifa ya Ulaya.

Aidha kiongozi huyo wa kiroho amesema Rais Samia ameendeleza utamaduni uliokuwepo tangu utawala wa serikali ya awamu ya kwanza, chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere wa kukutana na wazee na viongozi wa dini katika mikoa,kukutana kwake na viongozi wakuu wa dini mkoani Mwanza pamoja na wa Kanda ya Ziwa kumeleta faraja kwa makundi hayo.

Kwa upande wake Sheikhe Label ,amesema jambo alilofanya Rais Dk.Samia kupeleka rasimu ya mkataba wa uwekezaji wa bandari bungeni halijawahi kufanywa na serikali zote za awamu tano,iwe ya uwekezaji,ununuzi wa ndege,ujenzi wa barabara,madaraja,meli, reli ya kisasa na ununuzi wa ndege,hivyo apewe nafasi.

Amesema Bunge ni chombo cha wawakilishi wa wananchi kwa vile wamepitisha rasimu ya mkataba huo bungeni Rais asionekane msaliti, apewe nafasi tujadili kwa staha bila kuondoka kwenye reli kwa maslahi ya nchi bila kubomoa nchi, kwa kuwa Tanzania ni yetu tunataka ipate mapato ijiendeshe,hicho ndicho wanachokiona kwa Rais Samia.

“Mjadala wa uwekezaji wa uendeshaji wa bandari ni kwa maslahi ya nchi, uwe wa kujenga na si kubomoa,tunawausia wanasiasa na viongozi wenzetu wa dini,wasiingize maslahi ya kisiasa, udini,rangi, ukabila na ukanda anakotokea mtu,” amesema na kuongeza kuwa 

“Tusichokonoe jambo linaloweza kuliangamiza taifa,wanasheria waendelee kuwaelimisha wananchi na nadhani kuna mapungufu ndiyo maana Rais akataka yakajadiliwe bungeni kuingiza ukanda na ukabila ilihali kuliwahi kuwepo mikataba ya uchimbaji wa madini na upakuaji wa makontena bandarini lakini haikuzua mijadala kama huu.

Amesema Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza imekuwepo muda mrefu ikiundwa na viongozi makini wenye uwezo na nafasi ya kupima mambo,kusakafia udugu na kutuma ujumbe kwa serikali na jamii kama ilivyo kauli mbiu ya tunaishi pamoja,tunakula pamoja,tunacheza pamoja katika nchi moja Iitwayo Tanzania.

Hivi karibuni Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akiwa jijni Arusha, amesema serikali haitadharau maoni na kuwataka Watanzania waendelee kuwa na imani na serikali pamoja na wawakilishi wao bungeni kwa sababu imejidhatiti kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi unaoendana na mahitaji kuliko ilivyo sasa kutokana na udhaifu.

Amesisitiza kuwa bandari haijauzwa isipokuwa serikali inataka kubadilisha mwekezaji ijiendeshe kwa ufanisi na tija zaidi kwani licha ya maboresho yaliyofanyika utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ni wa kiwango cha chini kulinganisha na bandari shindani za kikanda,hivyo kuikosesha nchi mapato ambayo yangetumika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na kusaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma za wananchi nchin

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani humu, Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, akisafakafia jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini humo, wakati wa mkutano wa viongozi hao leo baada ya kutoa tamkoa kuhusu uwekezaji wa uendeshaji wa bandari.