Na David John, TimesMajira Online
CHAMA Kikuu cha Ushirika (KACU ) wilayani kahama mkoani shinyanga kimewataka wakulima wa zao la tumbaku wilayani humo kutumia fedha wanazozipata kutokana na uuzaji wa zao hilo kujenga nyumba za kisasa na bora na kuachana na nyumba za nyasi ili kuendana na uhalisia wa kilimo cha zao hilo.
Kimesema kuwa wakulima wamekuwa wakiuza zao hilo na kupata fedha nyingi lakini wengi wao wanaishia kutumia fedha hizo kwenye starehe ikiwemo pombe.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho wilayani Kahama Juni 21,mwaka huu Kaimu Mwenyekiti wa KACU Tani Mwandu amesema kuwa ni vyema wakulima wakatumia fedha zao kwa kufanya maendeleo na kuboresha nyumba zao.
“Sitavumilia kuona mkulima wa zao la tumbaku anaendelea kuishi kwenye nyumba ya nyasi badala yake fedha atakazozipata akafanye jambo la kimaendeleo ikiwemo kujenga nyumba za bati ,”amesema Mwandu.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti huyo amewataka wakulima kutojihusisha na suala la utoroshaji wa zao la tumbaku badala yake watumie kampuni zilitoletwa na serikali kununua zao hilo.
Alifafanua kuwa kwasasa masoko ni mengi na hakuna sababu ya mkulima kutorosha tumbaku ambalo litamsababishia kupata hasara na kushindwa kunufaika na kilimo chake.
“Mimi kama Mwenyekiti naishukuru sana Serikali kwani ipo pamoja na sisi na inaendelea kutafuta masoko na inatuletea kampuni nyingine kweli na kampuni zinaendelea kuiunga mkono serikali kwani wananunua kwa ubora unaotakiwa,”amesema Mwandu.
Kuhusu pembejeo amesema kuwa kwa mwaka huu kulikuwa na ubora wa hali ya juu na wakutosha hawezi kusema kwamba kulikuwa hamna ubora kwani wastani wa kitaifa wa tumbaku ulikuwa dola mbili lakini mpaka sasa hivi kuna wastani wa dola 2.3.
Sanjari na hayo amewashauri wakulima wa zao hilo kuweza kujenga mabani mengi ya kutosha ili kuifanya tumbaku kuwa na ubora kwasababu kampuni zinaendelea kuingia Kahama kutakuwa na kilo nyingi zaidi.
Akizungumzia upande wa zao la pamba pia amewaomba wakulima wa zao hilo wailete chama kikuu cha ushirika ili wakimaliza kuchakata waweze kuwalipa malipo ya pili yaani(bonus) na matarajio yao kwa mwaka nikuzalisha tumbaku na pamba kilo milioni 25.
Pia ameshukuru serikali pamoja na Mrajisi wa Mkoa wa shinyanga Hilda Boniphace kwani wamekuwa wakishirikiana nao vizuri hivyo wako imara na amesema hawatavunja sheria yeyote wanalipa wakulima kwa asilimia 100 pamba watasimamia vizuri na fedha za taasisi mbalimbali zitakuwa salama.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa