November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Handeni washangilia kupata maji ya bomba Karne ya 21

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Handeni

WANANCHI wa mtaa wa Kwamagome na Hedi, Kata ya Kwamagome, Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupata maji ya bomba Karne ya 21.

Akizungumza mara baada ya Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaib Kaim kuweka jiwe la ufunguzi mradi wa maji Kwamagome Juni 18, 2023, Mwenyekiti wa Mtaa wa Hedi, Kata ya Kwamagome Omar Kilango amesema tangu dunia iumbwe hawajawahi kuona ama kupata maji ya bomba.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim akizungumza kabla ya kuweka Jiwe la Ufunguzi wa Mradi wa Maji Kwamagome Juni 18, 2023.

Kilango amesema wananchi wa Kata ya Kwamagome wameteseka kwa muda mrefu wakitafuta maji kwa umbali mrefu, hivyo kuwekewa mabomba kwenye mitaa yao ni muujiza,wanamshukuru Rais Dkt Samia na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trank Main (HTM).

“Toka dunia iumbwe hatujawahi kuona hili jambo la kupata maji ya bomba,kwetu ni maajabu,wananchi wa Kwamagome tumeteseka kwa muda mrefu tukitafuta maji kwa namna tunavyojua wenyewe,tunamshukuru Mama Samia,tunaishukuru HTM kwa kuweza kupata maji kwenye Mtaa wetu wa Hedi kwa Karne ya 21,”amesema Kilango.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa wanawake kwenye Kata ya Kwamagome baada ya kuweka Jiwe la Ufunguzi wa Mradi wa Maji Kwamagome Juni 18, 2023.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa, Kaim, amesema mradi wa maji Kwamagome umetekelezwa kupitia fedha za Uviko-19.

Mradi huo umetekelezwa na Mkandarasi Build All Contractors LTD kwa Mkataba Na. AE/093/2021- 2022/W/02 na kusimamiwa na wataalam wa HTM.

“Mradi ulianza kutekelezwa rasmi mnamo Novemba 17, 2021 na ulikamilika Septemba 15, 2022, ambapo lengo la mradi huu ni kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa mitaa ya Kwamagome na Hedi wapatao 4,664.

Mradi huu umegharimu zaidi ya milioni 261 kati ya fedha hizo, Serikali Kuu ni zaidi ya milioni 244, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira HTM zaidi ya milioni 11 na wananchi ni milioni 5,”amesema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza amesema kazi zilizopangwa na kutekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kuchimba kisima kirefu (Borehole), kujenga nyumba ya mitambo katika eneo la Vugiri (kwa Mzee Yakobo) palipo na kisima,kujenga tenki la maji lenye ujazo wa lita 100,000,ujenzi wa jumla ya vituo tisa (9) vya kuchotea maji katika vitongoji vya Makoka, Mgambo na Tuliani.

Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim kabla ya kuweka jiwe la ufunguzi wa mradi wa maji Kwamagome.

Pia shule ya Msingi Kwamagome, Togeza, Malela, Soni, Hedi Centre na Msoto kuchimba na kulaza bomba kuu
lenye urefu wa mita 2,047 kutoka katika kisima hadi tenki la maji,kuchimba na kulaza mabomba ya kusambazia maji yenye urefu wa mita 5,281 kutoka katika tenki la kuhifadhia maji, kufunga pampu ya maji katika kisima kwa ajili ya kusukuma maji kwenda katika tenki na ujenzi wa Valve Chambers tisa.

Mhandisi Mgaza amesema wanamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kuwapatia fedha za mradi huo ambao utakwenda kutatua changamoto ya maji katika eneo hilo na kufikia lengo la kumtua mama ndoo kichwani huku akiahidi kuendelea kuyatunza mazingira ili miradi ya maji iwe endelevu.

Akizungumza na wananchi hao waliofurika kwenye eneo la ufunguzi wa mradi huo, Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga, Mhandisi Upendo Lugongo, amewaomba wananchi kuchangia huduma ya maji huku wakitunza miundombinu ya maji, vyanzo vya maji na mazingira yake ili miradi ya maji iwe endelevu.