November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Visima saba kuondoa changamoto ya maji Korogwe

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Korogwe

MRADI wa uchimbaji visima virefu saba katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga utaondoa changamoto ya upatikanaji maji kwenye mji huo kwa kushirikiana na vyanzo vingine vya maji.

Hayo yamesemwa Juni 19, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza (kulia) akisoma taarifa kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim alipotembelea na kukagua mradi wa Uchimbaji Visima Virefu saba katika Mji wa Korogwe Juni 19, 2023.

Ambapo Mhandisi Mgaza anasimamia utoaji huduma kwa muda kwenye Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mji wa Korogwe (KUWASA), amesema mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji kwenye Mji wa Korogwe.a

Amesema mradi wa maji wa uchimbaji wa visima virefu saba katika Mji wa Korogwe unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Korogwe, unatekelezwa kwa njia ya manunuzi ya “Single Source” na kandarasi alipewa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kupitia kitengo cha uchimbaji visima na mabwawa (DDCA).

“Mradi huu unatekelezwa katika kata sita za Majengo, Magunga, Mtonga, Kwamsisi, Mgombezi na Bagamoyo. Mradi ulianza kutekelezwa Machi 11, 2023 na ulitegemewa kukamilika Mei 30, 2023, lakini kutokana na changamoto za upatikanaji wa mabomba ya kisima (Casing), mkataba umeongezewa muda wa mwezi mmoja hadi Juni 30, 2023” amesema Mhandisi Mgaza.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa Abdallah Shaib Kaim (katikati) akipanda mti mara baada kutembelea na kukagua Mradi wa Uchimbaji Visima Virefu saba katika Mji wa Korogwe Juni 19, 2023. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Dkt. Alfred Kimea (kulia).

Mhandisi Mgaza amesema lengo la mradi huo ni kuongeza uzalishaji wa maji ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Mji wa Korogwe., ambapo gharama ya mradi ni zaidi ya milioni 230 ambazo ni fedha kutoka Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF).

Amesema kazi zilizopangwa na kufanyika ni pamoja na kufanya tathmini juu ya upatikanaji wa maji chini ya ardhi (Geological Survey) katika maeneo sita ya Kwasemangube, Majengo, Kwakombo, Mgambo,Manzese na Mtonga.

“Uchimbaji wa visima virefu sita katika maeneo ya Kwasemangube lita 36,000 kwa saa,Majengo lita 39,241 kwa saa,Kwakombo lita 48,000 kwa saa,Mbeza Mawe lita 38,156 kwa saa, Mgambo kilikosa maji, Manzese na Mtonga upimaji bado haujafanyika na kufanya vipimo vya ubora wa maji (Water Quality reports) katika maeneo ya Kwasemangube, Majengo, Kwakombo na Mbeza Mawe,” amesema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza amesema tathmini ya ubora wa maji katika visima vilivyopimwa inaonesha kuwa maji hayo yanafaa kwa matumizi ya binadamu.

Na mradi huo umeleta tija katika jamii kwa kuongeza ajira za muda mfupi na pia umeongeza uzalishaji wa maji katika Mji wa Korogwe kwa lita za ujazo 132,000 kwa siku.

“Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za mradi huu ambao utakwenda kutatua changamoto ya maji katika Mji wa Korogwe na kufikia lengo la kumtua mama ndoo kichwani,tutaendelea kuyatunza mazingira ili nayo yatutunze,”amesema Mhandisi Mgaza.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa alitembelea na kukagua kisima cha Majengo ikiwa ni moja kati ya visima saba vilivyochimbwa katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Korogwe.