-Mmoja avuliwa wadhifa, wengine kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao kwa miaka mitatu.
Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Tunduma.
WATUMISHI sita katika Halmashauri ya Mji Tunduma , Wilayani Momba wamefukuzwa kazi na wengine wawili wakikumbwa na adhabu ya kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kupatikana na makosa mbalimbali yakiwemo ya ubadhirifu.
Halmashauri hiyo pia imemshusha wadhifa Mkuu wa idara ya Kilimo wa Halmashauri hiyo, Ronald Msangi, huku watumishi wengine wanne wakinusurika baada ya kushindwa kupatikana na hatia katika makosa yaliyokuwa yakiwakabili,
Uamuzi huo ulifikiwa mwishoni mwa wiki na baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo katika kikao cha baraza malum mara bada ya kujigeuza kama kamati kwa lengo la kupitia na kujadili mashauri mbalimbali ya kinidhamu yaliyowasilishwa kwenye kikao hicho, ikiwemo ya ubadhirifu.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayoub Mlimba aliwambia wandishi wa habari kuwa, baraza hilo lilifikia uamuzi huo kufuatia hoja zilizoibuliwa na madiwani katika baraza lililopita la mwezi wa Disemba mwaka 2022.
“Baraza la madiwani katika mji wa Tunduma leo tumejigeuza kama kamati kwa mujibu wa sheria na kanuni tulizonazo ili kuweza kupitia mashauri mbalimbali ya watumishi waliofanya vibaya katika nafasi za utumishi wao, makosa yao yametokana na ubadhirifu wa mali za umma katika miradi yetu mbalimbali ya maendeleo, hivyo kama baraza tumefanya uamuzi kwa haki bila kumuonea yeyote” alisema Mlimba.
Mlimba alisema watumishi hao waliochukuliwa hatua walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili, ambapo kundi la kwanza ni la watumishi wa halmashauri walio katika ajira za kudumu na wale wa ajira za mkataba.
Aliwataja watumishi wa ajira za kudumu waliofukuzwa kuwa ni Mkuu wa kitengo cha manunuzi wa Halmashauri hiyo, Obeid Mwakalinga, Ofisa manunuzi daraja la pili, Ibrahim Lulimo, Mhandisi daraja la pili, Aly Farayo, pamoja na Dickson Kisemine ambaye ni mhandisi daraja la pili.
Aliwataja watumishi wengine wawili waliofukuzwa kazi ambao walikuwa kwenye ajira za mkataba katika Halmashauri hiyo kuwa ni Aly Hasan ambaye alikuwa Mhandisi wa majengo, pamoja na Japhet Chota ambaye alikuwa Mhadisi ukadiriaji majenzi katika Halmashauri hiyo.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mlimba alisema katika kikao hicho, watumishi wawili ambao ni Patricia Mbigili ambaye ni Ofisa elimu Sekondari katika Halmashauri hiyo na Raphael Simkonda (ofisa Mtendaji daraja la tatu) wao wamepewa adhabu ya kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao katika kipindi cha miaka mitatu.
Katika hatua nyingine, Baraza hilo limetoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmahauri hiyo ya Mji Tunduma, Philemon Magesa kuhakikisha kwamba kabla ya kuwarudisha kazini watumishi ambao hawakukutwa na hatia, wakiwemo waliopewa adhabu ya kukatwa mishahara yao, lazima andae kikao cha pamoja kati ya watumishi hao na kamati ya fedha ili kuwekana sawa.
More Stories
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua