November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi wa vyuo watakiwa kuwa mabalozi wazuri wa kutunza mazingira

Na Queen Lema, Timesmajira Online, Arusha

Wito umetolewa kwa wadau wa elimu hasa vyuo kuhakikisha kuwa wanatenga muda wa kuyajenga na kuelimisha jamii dhidi ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Hayo yameelezwa na Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini Lewis Nzali ambapo wakati akizungumza na wanafunzi wa chuo cha St.Agustine mkoani Arusha kwenye wiki ya mazingira.

Lewis amesema kuwa vyuo navyo ni sehemu mojawapo ya kuhimiza jamii hasa kutunza mazingira kwa kuwa mabalozi wazuri.

Alifafanua kuwa wanafunzi wa vyuo kama watafanya vyema na kuhamasisha jamii kuweza kuyatunza mazingira basi elimu hiyi itasambaa kwa haraka hivyo mazingira yatabaki salama.

“Tulikuwa hapo St.Augustine tumehamasisha utunzaji wa mazingira vyema lakini pia tumehamasisha hata hao wana chuo kuhakikisha kuwa wanakuwa na tabia ya kuelezea umuhimu wa kutunza mazingira sanjari na matumizi sahihi ya vyanzo vya mazingira,”.

Wakati huo huo alitoa wito kwa vyuo vingine kuhakikisha kuwa wanakuwa na klabu za mazingira ambazo nazo zitaweza kuchochea utunzaji wa mazingira hasa kwenye vyuo na jamii ambayo inawazunguka.

“Leo hapa chuoni tumeweza kufaya hii siku kwa kuwa wana klabu ya mazingira sasa vyuo vingine navyo vinatakiwa kuiga mfano huo wa kuwa na klabu ya mazingira,”amesema Lewis.

Amesema kuwa NEMC itaendelea kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya utunzaji mzuri wa mazingira ikiwa ni pamoja na kufanya makongamano kwenye vyuo na taasisi za elimu lengo likiwa ni kuutangaza umuhimu wa kutunza mazingira.