November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi zaidi ya 400 wapimwa afya bure na ALMC

Na Queen Lema Arusha

Hospitali ya Arusha Lutheran Medical center imefanikiwa kuwapima pamoja na kutoa elimu ya magonjwa yasioambukiza kama vile shinikizo la damu pamoja na kisukari kwa wananchi zaidi ya 400 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoani Arusha

Zoeli hilo la upimaji limefanyika kwa siku 2 mbali na kupimwa wananchi wamepewa elimu ya kuzingatia mlo sahihi.

Akiongea na vyombo vya habari mara baada ya kumalizika kwa kliniki hiyo Msaidizi wa Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo Michael Charles amesema kuwa wao kama hospitali wameamua kufanya kliniki hiyo dhidi ya magonjwa hayo Kwa kuwa bado elimu inaitajika.

Ameongeza kuwa magonjwa kama sukari na shinikizo la damu yamekuwa yakiwatesa sana wanajamii kutokana na magonjwa hayo kukosa dalili za awali.

“Sisi hapa tumeamua kuweka kambi hii kwa siku mbili ili wananchi waweze kupimwa na kupewa ushauri bure kabisa ili waweze kujikomboa kwa kuwa haya magonjwa yanasumbua sana hasa familia pale yanapotokea,”amesema.

Wakati huo huo alitoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa kila mara wanajiwekea utaratibu wa kupima afya zao kwa kuwa magonjwa mengine hayana dalili Kwa haraka.

“Unapopima mara kwa mara unaweza kujua maendeleo ya afya yako lakini pia unapata ushauri kutoka kwa wataalamu tofauti na pale ambapo unapofika hospitali wakati ugonjwa umeshakolea ndani ya mwili,”.

Pia alitoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa kila mara wanakula vyakula ambavyo ni sahihi na kuachana na tabia ya kula vyakula ambavyo vinehifadhiwa katika majokofu.

Amesema kuwa vyakula ambavyo vimeifadhiwa katika majokofu vinapoteza ubora na wakati mwingine vinasababisha hata ongezeko la magonjwa lakini kama jamii itakuwa inakula mlo sahihi ni rahisi sana kuepukana na magonjwa kama hayo.