Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Kahama
UJENZI wa shule ya sekondari ya wasichana wenye vipaji maalumu ya Bulyanhulu iliyopo kijiji cha Busulwangiri Kata ya Bulyanhulu Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga unatarajiwa kuinua uwezo wa watoto wa kike kufikia malengo na ndoto zao katika elimu.
Hali hiyo inatokana na uamuzi wa Mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu uliopo wilayani Kahama kuamua kujenga shule mpya ya sekondari ya wasichana kwa gharama ya milioni 800 huku lengo ikiwa ni kuwasaidia watoto wa kike kufikia malengo yao kwenye elimu.
Kaimu Meneja wa Mahusiano ya Jamii katika Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo amesema ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi katika jamii.
Hivyo katika shule hiyo wamejenga vyumba vya madarasa 12 ikiwemo jengo la utawala, nyumba mbili za walimu na bweni.
“Bweni ambalo limejengwa litakuwa na uwezo wa kubeba wasichana themanini kwa wakati mmoja, shule hii itakuwa ni ya wasichana wenye vipaji maalumu kutoka katika Wilaya yetu ya Kahama, tunaamini shule hii itakuwa nzuri na wasichana watafikia malengo yao kwa asilimia 100,” amesema Zuwena na kuongeza kuwa
“Tunaamini tutapata wataalamu kwa sababu shule tumeijengea maabara ya sayansi, chumba cha bailojia, kemia na fizikia kwa gharama ya milioni 800 na hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na itaanza kupokea wanafunzi Januari mwakani,”.
Amesema wanaamini wasichana watakaosoma katika shule hiyo watafikia malengo yao vizuri na watakapokuwa katika bweni wataepuka vishawishi mbalimbali pamoja na kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu wa kutoka nyumbani kwenda shuleni ambapo njiani hukutana na vitendo mbalimbali vya ukatili.
“Wasichana wengi wanapotembea umbali mrefu kwenda shule njiani hutendewa vitendo vya ukatili vinavyoweza kusitisha ndoto zao za kumaliza shule na kufikia lengo fulani, changamoto ya mimba za utotoni, maana kwa muda wote watakuwa bwenini chini ya uangalizi wa Mwalimu mlezi (matroni),”ameeleza.
Mbali na ujenzi wa shule mpya ya Busulwangiri pia mgodi huo wa Barrick Bulyanhulu umejenga bweni lingine katika shule ya sekondari ya Bugarama lenye uwezo wa kuchukua watoto 80 kwa wakati mmoja ikiwemo nyumba ya matroni atakayewasimamia watoto ili waweze kwenda vizuri katika masomo yao.
Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Bugarama, Christopher Simwimba amesema ujenzi wa bweni la wasichana katika shule yake pamoja na uzio utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha watoto wa kike kusoma kwa ufanisi pasipo hofu yoyote ya kutendewa vitendo vya ukatili wakiwa njiani kuja ama kutoka shuleni.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Bulyanhulu wameushukuru uongozi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa maamuzi yake ya kujenga shule hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa utapunguza changamoto ya watoto wa kike kushindwa kumaliza masomo yao.
James Mukasa ambaye ni mmoja wa walimu wa shule ya sekondari Bulyanhulu, amesema ujenzi wa shule hiyo ya wasichana wenye vipaji maalum utawakomboa watoto wengi wa kike na watafikia malengo yao waliyoyakusudia.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Busulwangiri Selali Gratian,amesema jamii katika kijiji hicho ilijitolea kununua eneo la ardhi ambalo shule hiyo imejengwa na kwamba wakazi wengi wa kijiji chake wameushukuru mgodi huo kwa uamuzi wa kuwajengea shule hiyo.
Kwa upande wake aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Charles Fusi ameishukuru serikali ya Rais kwa kuhimiza suala la uwepo wa mahusiano mazuri kati ya wazawa na wawekezaji nchini.
Amesema mgodi wa Barrick Bulyanhulu umefanya mambo mengi katika Halamshauri yake kupitia fedha za CSR wanazotoa kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati, vituo vya afya na upande wa sekta ya maji.
“Wenzetu hawa wametusaidia mambo mengi katika halmashauri yetu maana mbali ya ile inayotekelezwa kwa fedha za CSR lakini wamekuwa pia wakitekeleza mingine nje ya CSR, nitowe wito kwa wananchi wa Msalala wahakikishe miradi yote inayotekelezwa na Barrick basi itunzwe vizuri ili iwe endelevu,”ameeleza Fusi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa