November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mshambuliaji Mkongo wa Yanga SC, David Molinga ‘Falcao’ akiruka mazoezini leo kujiandaa na mpambano wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Picha na Mtandao.

Vigogo Yanga wamshangaa Zahera

Na Nuru Mkupa

VIGOGO wa klabu Yanga wamemjia juu aliyekuwa kocha wao Mwinyi Zahera kufuatia kauli na maoni yake anayoendelea kuyatoa kuhusu klabu hiyo ambayo yameonekana kuwakera.

Toka ameondoka ndani ya klabu hiyo kocha huyo amekuwa akitoa mtazamo wake juu ya mbao mbalimbali yanayofanywa na klabu hiyo ikiwemo kutaja baadhi ya wachezaji wanaopaswa kuondoka na wale wanaotakiwa kubaki kwenye timu hiyo.

Hivi Karibuni kocha hupo pia amenukuliwa akisema kuwa mshambuliaji, David Molinga hatokuwa katika kikosi cha timu hiyo msimu ujao kwani tayari ameshapata timu nyingine atakayojiunga nayo msimu ujao.

Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera aliyehusika katika usajili wa mshambuliaji Molinga amesema nyota huyo tayari amepata timu anachosubiri ni mkataba wake Yanga kumalizika ili aondoke.

Pia kocha huyo alisema kuwa, kinachokuondoa Molinga katika timu hiyo ni kutokuwa na furaha kutokana na baadhi ya tuhuma na kejeli anazotupiwa na mashabiki na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.

Lakini pia hii si mara ya kwanza kwa mchezji huyo kuhusishwa kuondoka ndani ya klabu hiyo kwani tayari Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela alishawahi kuthibitisha kuwa walishaanza mazungumzo ya kuvunja mkataba na Molinga aliyeshindwa kufikia malengo kwa mujibu wa mkataba wake wa miaka miwili.

Hata kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili tayari viongozi wa klabu hiyo walikuwa na mpango wa kuachana na Molinga lakini baadaye kocha Eymael aliamua kumbakiza ili kumsaidia japokuwa hayaweza kufikia malengo ya klabu.

Akizungumza na Majira kingozi huyo alisema kuwa, wao kama viongozi hawawezi kufuata maneno ya kocha huyo kwani kwa sasa wana kocha mpya Luc Eymael ambaye kwa sasa tayari ameshatoa mapendelezo yake ya wachezaji anaowataka kwenye kikosi msimu ujao.

Alisema, kama Molinga ameongea hayo kuwa hana furaha ndani ya kikosi cha Yanga basi ni ruksa kwake kuondoka na kuelekea kule anapopataka kikubwa ni kuongea na uongozi ambao ndio alioingia nao makubaliano .

Kiongozi huyo alisema kuwa, kwa sasa kocha huyo aache kuwavuruga kwani wanachokiangalia ni namna gani wanaweza kufanikisha mapendekezo ya aliyoyatoa kocha wao ili kuhakikisha wanakuwa na kikosi bora kitakachoweza kutoa ushindani mkali katika mechi za Ligi.

“Kwa sasa tunaangalia ni namna gani tutaimarisha kikosi chetu kuelekea msimu ujao na kuwa na kikosi imara. Kwa sasa tayari ripoti ya mwalimu ipo mezani na imeshaanza kutekelezwa na tutahakikisha tunafuata na kutekeleza yale yote anayoyahitaji,” alisema kuongozi huyo.

Siku chache zilizopita, klabu ya Yanga kupitia kwa Afisa Habari wake, Hassan Bumbuli  alisema kuwa, katika ripoti hiyo mwalimu ametaka viongozi wasajili haraka wachezaji wanne wa kimataifa ambao amewapendekeza kuongezwa katika kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.

Alisema kuwa, miongoni wachezaji waliopendekezwa na kocha Eymael ni mshambuliaji, kiungo, winga na beki ambao watachukua nafasi za wale watakaoondoka jambo ambalo limewaaminisha mashabiki wengi wa klabu hiyo huenda wakaachana na mshambuliaji  kutoka Ivory coast, Yikpe Gnamien ambaye ameshindwa kuonesha kile walichokihitaji.

Pendekezo hilo la mwalimu kutaka mshambuliaji ni wazi kuwa Yikpe hatokuwa tena na nafasi ndani ya klabu hiyo lakini wasiwasi pia ukiwa kwa David Molinga ambaye ameonekana kutokuwa na mahusiano mazuri sana na kocha Eymael.

Bumbuli alisema kuwa, kinachofanyika sasa hivi ni kufanyia kazi mapendekezo ya mwalimu kwa ufanisi mkubwa ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima ndani ya benchi lao la ufundi.

Akizungumzia wachezaji wa ndani wa klabu hiyo, Bumbuli alisema kuwa, kwa sasa mwanasheria wao ambaye ni Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama pa moja na Katibu Mkuu wao Dkt. David Ruhago anazungumza na wachezaji wa ndani ambao mwalimu amependekeza wabaki ndani ya kikosi hicho na mambo yatakapokaa sawa basi majina ya watakaoachwa yatawekwa hadharani.

“Kwa wale wachezaji wa ndani ambao mikataba yao inaelekea ukingoni tayari wameshaanza mazungumzo na viongozi lakini pia pale mda utakapofika wale wote ambao mwalimu amependekezwa kuachwa watawekwa hadharani,” alisema Bumbuli.