November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Holyland yaweka mikakati kupambana na ulawiti,usagaji na ushoga

Na Esther Macha,Timesmajira, Online,Chunya

KATIKA kukabiliana na vitendo vya ulawiti ,usagaji, ushoga ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya watu wasio na uadilifu, uongozi wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Holyland iliyopo Makangolosi Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imeweka mikakati kabambe ya kupambana na vitendo hivyo.

Mkurugenzi wa shule ya Holyland , Lawena Nsonda (Baba mzazi )akizungumza na Timesmajira jinsi walivyojipanga kukabiliana matukio ya ushoga , ulawiti na usagaji ambavyo vimekuwa vikifanywa na watu wasiokuwa na maadili mema kuwa wameweka masomo maalum ya kuelezea ubaya na dhambi ya vitendo hivyo.

“Tumekuwa na masomo ambayo yanayoendelea shuleni hapa ya kuelezea ubaya wa dhambi ya ulawiti , usagaji na ushoga tunawasomea watoto maandiko ya kwenye biblia juu ya Sodoma na Gomola ilivyoangamizwa kwa sababu ya matukio kama haya,”ameeleza Nsonda na kuongeza kuwa

“Pia tunawaeleza kuwa magonjwa mbambali yasiyo na tiba yatatokea na mvua kutonyesha , hivyo watoto wenyewe huogopa na kukemea dhambi za namna hiyo ,shule yetu inaendeshwa kwa misingi ya kidini na watoto wanajifunza kukemea tabia za namna hiyo,”.

Nsonda amesema wameendelea kukemea na kuweka mikakati mikubwa dhidi ya matukio hayo ambapo kuhusu mabweni shule hiyo ilipata kibali kutoka kwa Kamshna wa elimu nchini.

Amesema kuna usimamizi wa walezi wa watoto pamoja na uangalizi maalum ambapo mabweni ya watoto wa kike yapo mbali na ya wa kiume pia ya watoto wa kubwa darasa la sita na saba wanalala mabweni tofauti na watoto wadogo wa darasa la tano kushuka chini.

“Watoto wakiwa wanaogeshwa kwenye mabweni kunakuwa na walimu ili kuhakikisha hakuna michezo yeyote ya ukosefu wa maadili,”amesema.

Sanjari na hayo ametoa wito kwa wazazi na wakurugenzi wa shule kutoruhusu watoto kuangalia katuni , tamthilia ambazo zinafundisha mambo ya ushetani,kujamiana wenyewe kwa wenyewe.

Pia amesema serikali imepiga marufuku vitabu aina 16 ambavyo vilikuwa vinahamasisha mambo ya ushoga hivyo huo ni ushetani ambao umeingia na kufanya kazi na kwamba hayo mambo yalikuwa yanasikika duniani lakini sasa yameingia nchini hata hivyo shule hiyo inakemea kabisa tabia hiyo.

“Tunaendelea kujifunza kuwa huu ni mpango wa shetani, kuna baadhi ya vyakula vinaletwa vinamfanya mtoto kuwa na hisia za kufanya mapenzi au,tumeweka kizuizi kwenye geti la shule,tuna usalama vyakula tunalima wenyewe ili madawa kama yatapenyezwa yasiingie shuleni kwetu ,wazazi kuweni makini kwani dawa zikiwekwa kwenye chakula mtoto anatamani ushoga tunapaswa kuliombea taifa letu,“amesema.

Kwa upande wake Mkazi wa Makongolosi wilayani Chunya , Afred Bwaga amesema kuwa kuhusu ushoga na usagaji elimu zimekuwa zikitolewa katika shule mbalimbali ili kukabiliana na matukio hayo kwa watoto wadogo.

Askofu wa Kanisa la Kirutheri Afrika Mashariki Dkt. Edward Mwaikali amesema kuwa ushoga ni adui mkubwa wa uumbaji wa Mungu zamani ilikuwa Ulaya, Marekani dhambi ya ushoga ipo nchini kwa vijana na majirani zetu.

Katika mahuburi wachungaji , wazee wa kanisa waendelee kukemea kwa nguvu zote na wasipofanya dhambi hiyo italiangamiza taifa .