Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
MBUNGE wa Mvumi ,Livingstone Lusinde (CCM) amemuwakia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe kwa kauli yake kwamba Mkataba wa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai katika uendeshaji wa bandari una viashiria vyote vya kuhatarisha usalama wa Nchi kiuchumi na kisiasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Alhamisi Juni 8,2023, Jijini hapa,Mbunge huyo ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) Taifa, amesema alichokisema Mbowe hakikubaliki kwani kinaleta ubaguzi.
Jana Jumatano Juni 7,2023,Mbowe alitoa tamko akiwa nchini Italia ambapo alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa azimio hilo bungeni kwa dharura ili kupisha mashauriano ya muafaka wa kitaifa juu jambo hilo nyeti.
Lusinde amesema kuwa Mkataba huo kutokuwekwa wazi, Serikali inafanya mambo yake kwa siri na haiwezi kila kitu kukiweka wazi.
“Kauli hii inaweza ikaharibu Muungano kwanini Bandari ya Zanzibar haihusiki haya ni maneno ambayo sio ya kiungwana,Mbowe anataka kutuaminisha ni kosa Rais na waziri kutoka Zanzibar huu ni ubaguzi.”anahoji
Amesisitiza Rais akitoka Kilimanjaro mipaka yake ya kutoa maamuzi ihusu milima tu? vitu vingine visigushwe, asizungumze kuhusu Korosho azungumzie Kilimanjaro tu haiwezekani ?amehoji Mbunge huyo.
Kuhusu madai ya kuwemo kwenye ziara ya Wabunge waliosafirishwa kwenda nchini Dubai kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali Mbunge huyo amesema : “Sio kweli mimi sikwenda Dubai huo ndio uzushi wenyewe mimi nilikuwa namuuguza mke wangu alikuwa amelazwa India,”amesema.
Mbowe aliwataka wawakilishi wa wananchi kutopitisha azimio hilo hadi uwepo wa uelewa kwani kupitisha kwao ni kuruhusu michakato mingi kuendelea.
Leo Alhamisi Juni 8,2023,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa alinukuliwa na Vyombo vya habari akisema makubaliano ya ukomo wa muda wa mkataba baina yake na kampuni ya Duban Port World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai haujawekwa wazi hadi bunge litakapopitisha azimio lake kuhusu ushirikiano huo.
Hata hivyo Spika Dkt.Tulia Akson mapema leo bungeni alisema azimio la Bunge kuhusu kuridhia ushirikiano wa uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari Tanzania, litawasilishwa bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.
Azimio hilo ni mapendekezo ya kuridhia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa Bandari Tanzania la 2023.
Mbunge huyo amesema kuwa amewasikia ACT Wazalendo kupitia Zito Kabwe bila shaka uchambuzi wao ni wa kitaifa zaidi na wenye nia njema kuliko Mbowe,Mbowe anasema Rais anatoka Zanzibar na Waziri anatoka Zanzibar ila bandari ni ya Dar es Salaam
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi