Na.Penina Malundo
SERIKALI imetia saini Mkataba wa kufanya Tathmini ya Athari ya Kimazingira na Kijamii kwa ajili ya Ununuzi wa Meli za Uvuvi , Kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP).
Akizungumza mara baada ya kutia saini mkataba huo jana Jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonaz amesema mkataba huo ,utawezesha kufanyika kwa tathmini ya athari ya mazingira pamoja na matengenezo ya meli zitakazotumika katika uvuvi wa bahari kuu ili kupata mazao ya bahari yatakayochangia katika uchumi wa nchi.
Dkt. Yonaz ameendelea kusema kuwa, sambamba na tathmini hiyo pia utafanyika upembuzi yakinifu katika kuundwa kwa vyombo hivyo kazi itakayofanyika kwa muda wa siku 75 ambapo itagharimu kiasi cha sh. Milioni.
“Tanzania inazo rasilimali nyingi za majini, sasa ili kuhakikisha tunainua uchumi kupitia Uchumi wa Bluu Serikali imeona ni muhimu kutengeneza meli kubwa zitakazovua katika kina kirefu ili kupata mazao ya bahari ambapo meli nne zitatengenezwa kwa ajili ya Zanzibar na Meli tano kwa Tanzania Bara hivyo kukamilika kwake kutasaidia kuinua uchumi wa Taifa,’’amesema Dkt. Yonazi.
Amewahimiza wadau wa uvuvi ambao ni Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Shirika la Uvuvi la Zanzibar (ZAFICO) kushirikianana Mkandarasi huyo kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kikamilifu huku akihimiza kila mmoja kuwajibika kwa sehemu yake kwa lengo la kupata matokeo chanya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ushauri wa masuala ya Mazingira (TANSEQ), Lusako Raphael amebainisha kwamba lengo la kufanya tathimini hiyo ni kuhakikisha mradi hausababishi athari hasi katika mazingira na jamii.
“Mradi huu unalenga kuwezesha ununuzi wa meli pamoja na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata samaki hivyo tunategemea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote kama ZAFICO, TAFICO na Wizara ya Kilimo,”amesema na kuongeza
‘’Pia kuna mkakati wa kudhibiti athari za mazingira ambao ndiyo utakuwa muongozo wa utekelezaji wa mradi,’’amesema.
Ikumbukwe kuwa AFDP ni mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ukifadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi