Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online, Korogwe
BAADHI ya wananchi wa Wilaya za Korogwe na Handeni mkoani Tanga wamefurahia huduma ya bure ya matibabu ya macho hasa mtoto wa jicho.
Huduma hiyo ilihusisha vipimo, dawa, miwani, ushauri na upasuaji mdogo, na wenye matatizo makubwa walipewa rufaa ya kwenda hospirali kubwa za Bombo, Tanga, KCMC, Kilimanjaro na Muhimbili, Dar es Salaam.
Ni baada ya huduma hiyo kutolewa kwa siku nne kwenye Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga na Taasisi ya Al At ‘A Charitable Foundation Tanzania (ACF) ya jijini Dar es Salaam kwa ufadhili wa Taasisi ya Qatar Charity ya nchini Qatar.
Jalina Mswaki (32) kutoka Kijiji cha Kwemanolo, Kata ya Mgwashi wilayani Korogwe,amesema kuwa tatizo la mtoto wa jicho aliligundua miaka mitatu iliyopita ambapo alifanya jitihada za kupata huduma hii bila mafanikio kwa miaka yote mitatu, lakini leo anamshukuru Mungu wamekuja watu wa kuwapa huduma hiyo ya bure.
“Nipo kwenye foleni ya kwenda kufanyiwa operesheni ya mtoto wa jicho,Mungu akipenda nitaweza kurudi kwenye hali yangu ya kawaida,amesema Mswazi.
Naye Maimuna Msami (42) kutoka Kijiji cha Kweingoma, Kata ya Kwamatuku, Wilaya ya Handeni, amesema tatizo la mtoto wa jicho limemsumbua kwa zaidi ya miaka minne, kutokana na hali ya maisha, alishindwa kwenda kufanyiwa upasuaji hospitalini.
“Namshukuru Mungu baada ya kusikia kuna watu wamekuja Korogwe kutoa huduma ya macho, na vile Kweingoma ni karibu na Korogwe, nilipata taarifa hizo, na leo nipo hapa kwenye foleni ya kwenda kufanyiwa operesheni ya mtoto wa jicho,” amesema Msami.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Juni 5, 2023, Mratibu wa zoezi hilo kutoka Taasisi ya ACF, Aboubakar Mwinyimbegu, amesema zoezi hilo limefanyika kwa siku nne kuanzia Juni Mosi hadi Juni 4, mwaka huu.
Mwinyimbegu amesema zoezi hilo limekwenda vizuri na wamebaini tatizo hilo lilikuwa kubwa kwa Wilaya ya Korogwe, ambapo kwa siku hizo nne, zaidi ya wananchi 1,000 wamejitokeza kupima afya zao kati ya hao 109 wamefanyiwa upasuaji mdogo.
Haya hivyo mwaka jana kuna taasisi ilikuja Korogwe na kubaini kuna watu 167 wana matatizo ya mtoto wa jicho.
Hivyo baada ya kusikia hilo, ndipo taasisi yetu iliamua kuja Korogwe ili kuweza kupata fursa ya kuwasaidia wananchi kupata huduma hiyo.
“Tumefanya mambo manne kwa siku hizi nne, kwani tulianza na vipimo, kutoa dawa, miwani, ushauri na mwisho kufanya upasuaji mdogo,wananchi takribani 1,000 wamejitokeza kufanya uchunguzi huku109 wamefanyiwa upasuaji mdogo,”amesema Mwinyimbegu.
Mwinyimbegu amesema wamepokea ombi la Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo la kuwataka kurudi tena Korogwe, kwani tatizo hilo bado ni kubwa wilayani humo na wananchi wengi bado wana changamoto hiyo na hawajafikiwa na huduma hiyo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa