Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online, Shinyanga
MAHUSIANO kati ya Mgodi wa Almasi wa Mwadui uliopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga na wakazi wa kata tano zinazouzunguka yameimarika zaidi baada ya Mgodi huo kuongeza kiwango cha fedha inazotoa za CSR kusaidia miradi ya kijamii kwenye kata hizo.
Hali hiyo imebainishwa na wanavijiji wanaoishi kwenye vijiji 12 vinavyouzunguka Mgodi huo huku wakiishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhimiza suala la wawekezaji kuwa na mahusiano mazuri na wenyeji katika maeneo waliyowekeza miradi yao.
Wananchi hao wamesema hali ya mahusiano kati yao na mwekezaji Kampuni ya Williamson Diamonds Ltd kwa sasa imeimarika kutokana na kampuni hiyo kuongeza kiasi cha fedha inazozitoa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye vijiji vyao.
Diwani wa kata ya Mwadui-Lohumbo Francis Manyanda na Lwinzi Kidiga ambaye ni diwani wa kata ya Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wanasema kitendo cha kuongeza fedha za miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao kimemaliza uhasama uliokuwepo miaka ya nyuma kati ya Mgodi na wanavijiji.
“Nichukue nafasi hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka sera nzuri ambayo ndiyo imechochea maendeleo haya mnayoyaona katika vijiji vyetu vyote na kata kwa ujumla, kwa hatua yake ya kuwasukuma wawekezaji kufanya mrejesho wa fedha za maendeleo kwa wananchi,”
“Wakati Rais Samia akiingia madarakani, mwekezaji huyu Williamson Diamonds alikuwa akitoa shilingi milioni 150 za CSR kwa mwaka kwa vijiji 12 vilivyozunguka mgodi huu, lakini leo hii kwa sera nzuri za Rais tumeanza kupokea shilingi bilioni 1.200 kwa ajili ya miradi ya kijamii katika kata zetu, tunamshukuru sana Rais,” anaeleza Manyanda.
Kwa upande wake diwani Lwinzi anasema hivi sasa kata yake ya Maganzo inanufaika na fedha zinazotolewa na mwekezaji huyo ambazo zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika upande wa elimu na miundombinu ya barabara.
Lwinzi amesema mwaka huu wa 2023 kata yake imepokea zaidi ya shilingi milioni 260 kwa ajili ya utekelezaji wa miraji ya kijamii ambapo shilingi milioni 240 zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya ya mabasi cha Maganzo na shilingi milioni 13 zimeelekezwa kwenye utengenezaji wa barabara.
Naye Sara Marco ambaye ni diwani wa kata ya Idukilo anasema hatua ya mgodi wa Mwadui kuanza kusaidia miradi ya kijamii imesaidia kupunguza changamoto katika baadhi ya maeneo hasa upande wa sekta ya elimu, miundombinu ya barabara na afya.
“Kwa kweli tunaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo imekuwa ikihimiza suala la mahusiano mema kati ya jamii na wawekezaji wetu hapa nchini na pia tunaushukuru uongozi wa Williamson Diamonds Ltd wa Mwadui kwa misaada hii ya kijamii wanayotupatia,”
“Kwenye kata yetu wametupatia msaada wa kutujengea vyumba vinne vya madarasa na nyumba moja ya mwalimu, mwaka jana pia walitupatia shilingi milioni 13 ambazo kwa sehemu kubwa tumezitumia kwa ajili ya ujenzi wa matundu 14 ya vyoo kwenye shule ya msingi Mwangombolwa, tunawashukuru sana,” anaeleza Sarah.
Bernard Mihayo ni Meneja mahusiano katika Mgodi wa Williamson Diamonds Ltd ambaye anakiri kuimarika kwa hali ya mahusiano kati ya Mgodi na jamii inayouzunguka mgodi huo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma. moja ya mambo yanayopewa kipaumbele na kampuni yake ni kuimarisha mahusiano kati yake na jamii inayowazunguka.
Hata hivyo anasema hali ya uwekezaji kuendelea kuwa na nzuri na kuimarika kwa mahusiano kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ambayo inapotokea changamoto yoyote Serikali huonesha mchango wake kuhakikisha kazi zinaendelea kufanyika pasipo matatizo hali inayoonesha wazi Serikali, wawekezaji na jamii kwa ujumla kwa sasa wapo pamoja.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude anasema utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa jamii unaotekelezwa na Mgodi wa Williamson Diamonds Ltd. ni moja ya maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2023.
“Kwetu sisi kama Serikali tunamshukuru mwekezaji huyo kwa jinsi anavyotekeleza majukumu yake hasa katika suala zima la kusaidia jamii inayomzunguka wanaoishi kwenye vijiji 12 ambao hivi sasa wanapata misaada mbalimbali ya kijamii ikiwemo miradi ya kijamii, michezo na utunzaji wa mazingira,” ameeleza Mkude.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa