November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kujenga hospitali itakayotoa huduma za kibingwa Ukerewe

Na Judith Ferdinand, Timesmajira online, Ukerewe

Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuanza ujenzi wa hospitali yenye hadhi Mkoa wilayani Ukerewe mkoani Mwanza itakayokuwa na uwezo wa kutoa huduma za kibingwa nne ikiwemo huduma za kibingwa za upasuaji, upasuaji wa mifupa, za kina mama ya magonjwa ya uzazi na wanawake pamoja na magonjwa ya watoto.

Ambapo ukamilikaji wa hospitali hiyo utaweza kusaidia wakazi waishio katika visiwa 38 vilivyoko wilayani Ukerewe mkoani Mwanza ambao kutokana na jiografia ya eneo hilo iliwalazimu kuvuka maji kufuata huduma za kibingwa jijini Mwanza.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu,mara baada ya kukagua eneo la hekari 16 Kata ya Bulamba Kijiji cha Bukindo ambapo patajengwa hospitali hiyo yenye hadhi ya Mkoa yenye lengo la kuwaondolewa adha wanaukerewe ambao ulazimika kuvuka maji kufuata huduma hizo za kibingwa hospitali ya Sekou-Toure au Bugando jijini Mwanza.

Ummy ameeleza kuwa, sababu ya kujenga hospitali hiyo ni maamuzi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuona changamoto wanayoipata wananchi wa Ukerewe ambapo tayari serikali imeshatenga kiasi cha bilioni 4,kwa ajili ya ujenzi huo.

“Tunataka wanaukerewe wapate matibabu ya kibingwa ndani ya Ukerewe,siyo waende Mwanza na sisi Wizara ya tunaenda kujenga hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ukerewe kwa kujenga ghorofa moja au mbili lakini tuanze na moja kwanza,tunachotaka huduma za kibingwa zitolewe Ukerewe tuanze na hizi kada nne,sasa tukikamilisha angalau Ukerewe tutakuwa na madaktari bingwa wanne,”ameeleza Ummy na kuongeza kuwa

“Daktari atakuja na kuchukua taarifa ya miaka mitatu nyuma ili kujua rufaa zinazoenda Sekou-Toure na Bugando ni zipi hivyo baada ya hapo ndio tutajua hiki tunachotaka kufanya kinakidhi mahitaji ya wanaukerewe,”.

Pia amefafanua kuwa hospitali ya Wilaya ya Ukerewe ambayo ilitarajiwa kuwa ya Mkoa kwa sasa itaendelea kuwa hospitali ya Wilaya ambapo Hospitali ya Mkoa itajengwa katika Kata ya Bulamba kijiji cha Bukindo.

“Kwa kushirikiana na wataalam wangu nimeridhishwa na eneo hili sasa hatua ya uchoraji wa ramani unaanza ili kuwezesha kujua thamani ya ujenzi huo ambapo ujenzi wa hospitali hiyo unatarajia kuanza mapema iwezekanavyo,”.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Charlse Mkombe amesema hospitali hiyo itakapokamilika wananchi kati ya 15 hadi 20 wanaopewa rufaa kwenda kupata matibabu jijini Mwanza watatibiwa hospitalini hapo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amesema uongozi wa mkoa huo utasimamia vizuri ujenzi huo na kuhakikisha unatekelezwa kwa kiwango na wakati ili wananchi wapate huduma iliyokusudiwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile ameishukuru Serikali huku akiwahakikishia wananchi wa Ukerewe kuwa tutakuwa na hospitali nzuri yenye huduma zote muhimu hivyo hakutakuwa na haja ya kupanda tena boti kwenda Mwanza kufuata huduma za afya.

Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, Joseph Mkundi ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa hospitali hiyo na kuiomba itatue changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya wilayani humo.