November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana Tabora waunga mkono juhudi za Rais Samia

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

KIKUNDI cha Vijana na Maendeleo Mkoani Tabora kimeunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia mifuko 20 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya sh 450,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule ya msingi.

Msaada huo umetolewa juzi kwa shule ya msingi Mtakuja iliyoko katika kata ya Ntalikwa, halmashauri ya manispaa Tabora ambayo inakabiliwa na uchakavu wa vyoo na vyumba vya madarasa ili kuboresha mazingira ya shule hiyo.

Akikabidhi saruji hiyo Mwenyekiti wa Kikundi hicho Sara Wambura alisema msaada huo utasaidia kuboreshwa vyoo vya shule hiyo na vyumba vya madarasa na kuwaondolea wanafunzi adha ya kukosa sehemu ya kujisitiri .

Alisema kama vijana hawakuridhishwa na hali ya vyoo hivyo, hivyo wakaamua kuchangishana ili kupata kiasi fulani cha fedha kwa ajili kununua mifuko hiyo ili kufanikisha ujenzi wa vyoo vya kisasa shuleni hapo.

‘Tulipita hapa siku moja, kwa kweli hatukufurahishwa na hali tuliyoikuta, vyoo vilikuwa haviridhishi hali inayoweza kuhatarisha afya za wadogo zetu, tuliamua kwenda kuchangishana na leo tumekuja kukabidhi kile tulichopata’, alisema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Sophia Kaleza aliwashukuru vijana hao na kubainisha kuwa ni mfano wa kuigwa miongoni mwa jamii, walichokifanya ni kikubwa sana kwani kitasaidia kujengwa vyoo vipya.

Alitoa wito kwa wadau wengine kujenga utamaduni wa kujitolea kusapoti maendeleo ya jamii katika maeneo yao kwa kuwa serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu kwa wakati mmoja.

Diwani wa kata hiyo Osca Rioba alibainisha kuwa serikali kwa kushirikiana na wananchi tayari imeanza kuchimba shimo kwa ajili ujenzi wa matundu ya vyoo vya kutosha shuleni hapo.

Aliongeza kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 371ina matundu 10 tu ya vyoo ambayo licha ya kuchakaa bado hayawezi kutosheleza uhitaji wa shule hiyo, hivyo akaomba wadau wengine kujiotokeza kuwaunga mkono.  

Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana na Maendeleo cha Mkoani Tabora Sara Wambura (aliyeshika mkoba) akikabidhi mifuko 20 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya sh laki 4 kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mtakuja, kata ya Ntalikwa katika halmashauri ya manispaa Tabora kwa ajili ya ujenzi wa vyoo. Picha na Allan Vicent.  Â