November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waganga wa kienyeji 33 watiwa mbaroni

Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia waganga wa tiba asili 33 wakituhumiwa kufanya shughuli ya huduma ya tiba hizo bila usajili na kupiga ramli chonganishi huku vijana watano wa kiume wanaodaiwa kuingiliwa kinyume na maumbile pia wakinaswa katika mtego wa polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 26,mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Wilbroad Mutafunga amesema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti ya wilaya za Nyamagana, Kwimba, Misungwi,Magu, Sengerema na Ilemela.

Mutafungwa ameeleza kuwa waganga hao wa kienyeji wanaodaiwa kupiga ramli chonganishi na kufanya shughuli ya kutoa huduma ya tiba asili bila kufuata sheria kwani ramli chonganishi zimekuwa chanzo cha mauaji, majeruhi na ukatili wa kijinsia.

Amesema waganga hao wa tiba asili walikamatwa kwa nyakati tofauti kwenye msako wa kudhibiti vitendo vya kihalifu na mazalia ya uhalifu iliyofanyika katika Wilaya za Kwimba, Nyamagana, Misungwi, Magu,Sengerema na Ilemela kati ya Mei 17 hadi 24, mwaka huu.

“Wamekamatwa kwa nyakati tofauti wakiwa na vielelezo mbalimbali wanavyotumia kufanya shughuli za uganga wa jadi bila kusajiliwa,pia ramli chonganishi ni vitendo vinachochea mauaji,majeruhi na ukatili wa kijinsia,hivyo wananchi wajiepushe na waganga wa aina hiyo,”amesema Mutafungwa na kuongeza kuwa wamehojiwa na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha vijana tano wa kiume akiwemo mfanyabiashara mmoja wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja wamenaswa na polisi Mei 24, mwaka huu, kwa kosa la kuruhusu miili yao kuingiliwa kinyume na maumbile wakiwa katika saloon ya Uniquie huko Nyasaka,wilayani Ilemela.

Kamanda huyo wa polisi amewataja vijana hao ni Ramkhity Bailkhabaty (26) na Daniel Omary (24) wote wakazi wa Buzuruga, Ernest Malongo (20), mkazi wa Mecco, Jefta Joseph (27),mkazi wa Kiseke na mfanyabiashara Edward Abel maarufu Shija (30),mkazi wa Nyamuge, wote wa wilayani Ilemela na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.