Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kimeendesha mafunzo ya siku moja kwa wanahabari zaidi ya 25 kutoka Mikoa ya Singida, Shinyanga, Simiyu, Kigoma na Tabora ya namna ya kulinda usalama wao wakiwa kazini.
Akifungua mafunzo hayo jana Meneja Miradi na Mikakati wa TAMWA Sylivia Daulinge alisema usalama wa wanahabari ni jambo la msingi sana mahali popote wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Alibainisha kuwa ili kufanikisha majukumu yao ni muhimu sana kuchukua tahadhari ya viashiria vyo vyote vya usalama vinavyoweza kuhatarisha maisha yao ikiwemo kupoteza vifaa vyao vya kazi.
Alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa na kuwapa mbinu za kutambua hatari zilizoko mbele yao popote wanapokuwa na namna ya kujikinga wanapoteleza majukumu yao.
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Mwanahabari Mkongwe Edwin Soko alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kutokana na kuongezeka kwa matukio mabaya dhidi ya wanahabari na kukosekana kwa mifumo ya kujitosheleza kuwalinda.
Alisema wanahabari wanapaswa kutambua kuwa mazingira wanayofanyia kazi si salama hivyo kuchukua hatua madhubuti ili kupunguza matukio hasi yanayoweza kuwakumba wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Soko alitaja madhira wanayopata wanahabari kuwa ni pamoja na mauaji, kutekwa, kuteswa, kudhalilishwa, kunyanyapaliwa, kunyimwa taarifa, kunyang’anywa vifaa vya kazi ikiwemo vitisho (threats), udhaifu (vulnerability) na mengine mengi.
Alibainisha baadhi ya mbinu wanazopaswa kuchukua kuwa ni kupunguza vitisho, udhaifu na kuongeza uwezo wa kukabiliana na hatari zilizoko mbele yao ikiwemo kutoa taarifa punde kwenye vyombo vyao au mamlaka zingine wanapoona au kukumbana na madhira yoyote.
Aidha alieleza kuwa usalama upo wa aina 2 wa mtu binafsi na vitu (physical security) na wa kimtandao (digital security) hivyo akataka kila mmoja kuhakikisha anajilinda, kulinda vifaa vyake na kuwa makini anapotumia mitandao.
Soko alitoa mfano katika kipindi cha mwaka 2022 kuwa jumla ya wanahabari 18 hapa nchini walikumbwa na madhira mbalimbali ikiwemo vitisho, kutekwa, mauaji, kupotea, kudhalilishwa, kuwekwa ndani na mengineyo kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Aidha katika kipindi hicho kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Reporters Without Border (RSF) jumla ya wanahabari 57 duniani waliuawa, 65 walishikiliwa, 533 walifungwa na 49 walipotea, hivyo kuwepo haja ya wanahabari kuchukua tahadhari kubwa wanapotekeleza majukumu yao.
Mwajabu Kigaza, mmoja wa washiriki wa semina hiyo kutoka Mkoani Kigoma aliwapongeza TAMWA kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kuchukua tahadhari wakati wote na mahali popote wanapoenda kutekeleza majukumu yao.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti