November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyakazi CRDB watakiwa kuwa waaminifu, waadilifu na wabunifu

Na Yusuph Mussa, Arusha

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela amewataka wafanyakazi wa benki hiyo kufanya kazi kwa weledi, kujituma, uadilifu, uaminifu na ubunifu ili waendelee kuwa benki bora nchini, na inayotegemewa na wananchi.

Pia amesema atafanyia kazi ushauri, maoni, na maeneo ya kipaumbele ili kuweka matawi ya benki ikiwemo eneo la Holili na Njiapanda ya Himo mkoani Kilimanjaro ili kurahisisha huduma kwa wateja na wananchi.

Aliyasema hayo Mei 20, 2023 wakati anajibu hoja za wajumbe kwenye Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB jijini Arusha, ambao ulitanguliwa na Semina ya Wanahisa Mei 19, na shughuli za maendeleo na kijamii kwa siku mbili.

“Nataka niweke msisitizo kwa wafanyajazi. Mnatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu, ubunifu na weledi mkubwa ili kuweza kulinda mafanikio tuliyoyapata na kuendelea kuwa benki ya kuaminiwa na kutumainiwa na wananchi katika kutoa huduma.

“Pia tutachukulia kwa uzito mkubwa ushauri, maoni na hoja zilizotolewa ikiwemo kule Holili na Njiapanda ya Himo. Tunataka wateja wetu wasipate tabu kuitafuta huduma yetu, na ndiyo maana tunasema Ulipo Tupo” alisema Nsekela.

Awali, katika taarifa yake kwa wanahisa, Nsekela alisema benki hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano ikiwemo faida ya sh. bilioni 351 mwaka 2022, hivyo kuitaka menejimenti na wanahisa kushirikiana ili kulinda mafanikio hayo, na ikibidi, mwakani faida iweze kuongezeka.

“Mageuzi thabiti yanathibitishwa na taarifa zetu za fedha zinazoonesha, katika miaka mitano iliyopita, utendaji wa benki umekuwa ukiimarika licha ya changamoto kadhaa zilizotokea kwenye mazingira ya ufanyaji biashara hasa zikichangiwa na janga la UVIKO-19 na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine.

“Faida Baada ya Kodi imeongezeka kufika sh. bilioni 351 mwaka 2022 ikilinganishwa na sh. bilioni 36 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 875.
Na kutokana na ukuaji huo wa faida, thamani ya hisa imepanda sokoni, ambapo baada ya CRDB kutangaza matokeo yao ya hesabu za fedha hivi karibuni, hisa imepanda hadi sh. 510, ambapo mwaka 2017 bei ya hisa moja ya Benki ya CRDB ilikuwa sh. 90, na hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 567 ndani ya miaka mitano” alisema Nsekela.

Nsekela alisema alipokabidhiwa jukumu la kuongoza benki miaka mitano iliyopita, alidhamiria kutimiza matarajio kwa kuboresha utendaji wa kifedha wa benki, na kuhakikisha
wanakuwa na ukuaji endelevu katika biashara hiyo ingawa haikuwa rahisi, lakini leo anajivunia kuona
wanaweza kutazama nyuma walipotoka kwa furaha kubwa, wakitambua hatua kubwa waliyopiga katika kujenga benki imara na kiongozi katika soko.

“CRDB inashikilia nafasi ya benki kubwa zaidi ya biashara na benki kiongozi nchini, si kwa bahati mbaya bali kwa utashi, imani na kujitoa kwa wanahisa wetu, washirika, wafanyakazi na watu wengine wengi wenye nia njema na benki yetu. Ninawashukuru
wote kwa ushirikiano mnaotupatia, na ninaahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa kwa manufaa makubwa zaidi kwetu sote. Tafakari ya utendaji wetu miaka mitano iliyopita, inatoa taswira nzuri ya uwezo wa Kundi katika utendaji na uzalishaji wa matokeo chanya, licha ya changamoto katika mazingira ya nje ya biashara.

“Kundi linaendelea kuonesha matarajio makubwa ya kibiashara,
yakichagizwa na misingi thabiti na huduma na bidhaa madhubuti ambazo
zinazingatia mahitaji ya soko. Mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya utekelezaji
mzuri wa mkakati wetu wa muda wa kati 2018 -2022, uliojikita kwenye nguzo tatu:

  • Kuboresha miundombinu ya utoaji huduma
  • Kujenga Benki ya Kesho
  • Kuboresha mazingira ya utendaji/ ufanyaji kazi
    Tulipoanza safari hii mwaka 2018, kipaumbele chetu kilikuwa ni kuhakikisha utekelezaji wa makini wa mkakati wa miaka mitano ili kufkia uwezo kamili wa Kundi” alisema Nsekela.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay, akijibu hoja za wanahisa, alisema inawezekana faida kutoka sh. bilioni 351 hadi sh. bilioni 450, lakini na gawio kutoka sh. 45 kwa hisa moja hadi sh. 100 ikawezekana, ili mradi kuwe na uwajibikaji na ushirikiano wa pamoja kufikia malengo hayo.

Dkt. Laay amewataka menejimenti na wanahisa kutobweteka na mafanikio, kwani ushindani ni mkubwa, na wanatakiwa kuyalinda mafanikio hayo waliyoyapata kwa nguvu zote.

Dkt. Laay alisema taarifa za fedha kwa mwaka wa fedha unaoishia Desemba
31, 2022. ripoti hiyo inaangazia juhudi na mafanikio ya benki katika mwaka huu. Inaainisha pia hatua zao zijazo
wanapoendelea kujenga biashara thabiti yenye jukumu la kujenga thamani endelevu. Amewashukuru kwa dhati
wanahisa kwa msaada thabiti, ambao umeifanya benki hiyo kuwa kinara katika sekta ya fedha nchini. Kujitolea kwao
kwa maendeleo ya benki kunaakisiwa na namna ambayo wamekuwa wakishiriki na kusaidia ukuaji endelevu bila kuchoka.

“Kwa furaha kubwa ninawasilisha kwenu ripoti ya mwaka na taarifa za fedha kwa mwaka wa fedha unaoishia Desemba
31, 2022. Ripoti hii inaangazia juhudi na mafanikio ya Kundi katika mwaka huu. Inaainisha pia hatua zetu zijazo
tunapoendelea kujenga biashara thabiti yenye jukumu la kujenga thamani endelevu. Ninawashukuru kwa dhati
wanahisa wetu kwa msaada thabiti, ambao umeifanya Kundi
kuwa kinara katika sekta ya fedha nchini. Kujitolea kwenu kwa maendeleo ya benki kunaakisiwa na namna ambayo
mmekuwa mkishiriki na kusaidia ukuaji endelevu bila kuchoka, juhudi wanazoendelea kufanya katika kuhakikisha Kundi linabakia kuwa imara.

“Bodi ya Wakurugenzi
imejitolea kutoa usaidizi unaohitajika na
inaendelea kutekeleza jukumu lake la uangalizi katika kuongoza timu kutekeleza mkakati wake
wa biashara. Katika mwaka 2022, mtazamo wa Kundi ulijikita
katika kujenga thamani endelevu, kwa kuelekeza rasilimali katika miradi na uvumbuzi wenye athari kubwa kulingana na malengo ya muda mrefu. Kwa
ujumla, Kundi lilifanya uwekezaji mkubwa katika kuongeza ufkiaji wa huduma za kifedha kupitia
njia mbadala, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa mtandao wa benki kupitia wakala (CRDB Wakala) na kurahisisha ufunguzi wa akaunti kupitia simu za
mkononi. Kufuatia uwekezaji huu, Kundi lilifkia hatua nyingine kubwa kwa kuvuka kiwango cha mizania cha sh. trilioni 10″ alisema Dkt. Laay.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela, akitoa taarifa kwenye Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 20, 2023. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay, akitoa taarifa kwenye Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 20, 2023. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 20, 2023. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkutano Mkuu wa 28 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika jijini Arusha Mei 20, 2023. (Picha na Yusuph Mussa).