Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imesema,inatarajia kuanza kusajili shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa mfumo wa kielektroniki.
Akizungumza Bungeni jijini wakati akiwasilisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia ,Waziri wa Wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda amesema, lengo la kuongeza ufanisi na kuwafikia wadau wengi zaidi.
Amesema katika mwaka ujao wa fedha serikali inatarajia kusajili shule za msingi na sekondari takribani 560 huku za awali pekee zikiwa 20 na awali na msingi zipatazo 380 ambapo katika shule hizo zipo za serikali na zisizo za serikali
Aidha amesema,shule za sekondari 165 na chuo cha ualimu kimoja cha binafsi na nyingine kwa kuzingatia maombi yatakayowasilishwa na kukidhi vigezo vitasajiliwa pia.
“Tumepanga kufanya hivi ili kuwezesha ongezeko la fursa na Ubora wa Elimu ya Msingi na Sekondari na kupata wahitimu wenye sifa za kujiajiri na kuajirika.”amesema Profesa Mkenda
Aidha Waziri Mkenda ametaja vipaumbele vitano vitakavyotekelezwa katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024 ambayo vyote kwa pamoja na vinalenga kuongeza ubora wa elimu hapa nchini.
Profesa Mkenda amesema,utekelezaji wa vipaumbele hivyo pia utawezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.
Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu na kuanza utekelezaji,kuongeza fursa na ubora wa mafunzo ya amali (Ufundi) katika elimu ya sekondari na vyuo vya Kati vya Amali.
Vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na ubora wa Elimu ya Msingi na Sekondari, kuongeza fursa na ubora wa Elimu ya Juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika Utafiti, Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Kuhusu mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Eimu Waziri huyo amesema,hayo na kuanza utekelezaji wake kwa lengo la kuimarisha maarifa na ujuzi kwa wahitimu wa ngazi zote za elimu.
“ Sambamba na kukamilisha mapitio ya sera na mitaala ya elimu, Serikali itafanya mapitio na marekebisho ya sheria ya elimu kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na sheria mbalimbali za Taasisi za Elimu ili iendane na mahitaji ya toleo jipya la sera pamoja na mitaala,
“Vile vile itaandaa Mwongozo wa Chakula na Lishe pamoja na Mwongozo wa Utunzaji wa Mazingira katika Taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa lengo la kuhakikisha kuwa viwango vya utolewaji wa chakula katika vyuo vinatekelezwa ipasavyo na watoa huduma.
Aidha amesema, Serikali itaendelea kuboresha mafunzo ya Amali (Ufundi na Ufundi Stadi) kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu ambapo inakwenda kuwezesha ukarabati shule za sekondari za ufundi na kuzipatia vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia imeomba kuidhinishiwa zaidi ya Trilioni 1.675 mbapo kati ya hizo kiasi cha shilingi Trilioni 1.137 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ndani ya Wizara hiyo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa