Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
MADAKTARI bingwa wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wamefanikiwa kuwapatia matibabu ya kibingwa wagonjwa zaidi ya 724 wa moyo nchini Malawi walikoweka kambi ya siku tano.
Matibabu hayo yamefanikiwa chini ya uratibu wa Kamati ya Utalii Tiba inayoongozwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dk. Mohamed Janabi na Makamu wake, Abdulmalik Mollel, ambaye ni Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL).
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam jana, Kiongozi wa msafara wa madaktari hao ambaye ni daktari bingwa wa maradhi ya Moyo wa JKCI, Dk. Angela Muhyoza, alisema kambi hiyo ilianyika katika hospitali ya Qeen Elizabeth
Amesema walikuwa na madaktari bingwa wa watoto wawili na madaktari bingwa wa watu wazima wawili na wataalamu wengine waliokuwa wakiwasaidia madaktari hao.
Amesema kati ya wagonjwa waliowahudumia, 524 waligundulika kuwa na matatizo ya moyo ambapo baadhi yao walipatiwa tiba hapohapo wakati wagonjwa 200 walihitaji huduma za upasuaji mkubwa wa kufungua kifua.
“Miongoni mwa wagonjwa hao, 60 wanahitaji matibabu ya haraka kutokana na matatizo waliyonayo kwa hiyo wasipopata matibabu ndani ya muda huo wanaweza kupata matatizo zaidi, wananchi wa Malawi wamefurahia huduma zetu na walitamani tuendelee kuwepo nchini kwao,” amesema
Wakati huo huo, Serikali ya Malawi imeishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapeleka wataalam wa moyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa nchi hiyo.
Shukrani hizo zilitolewa na Waziri wa Afya nchini Malawi, Khumbize Chiponda alipotembelea Hospitali ya Queen Elizabeth kuangalia huduma zilizokuwa zikitolewa na wataalam wa afya kutoka (JKCI) wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo.
Khumbize amesema Malawi na Tanzania wamekubaliana kuwa na kushirikiano katika kujengeana uwezo kwani nchi hiyo bado haijaweza kuanzisha hospitali ya moyo hivyo kupitia kambi hiyo wataenda kujitathimini uwezo wao kama wanaweza kuanzisha kituo ambacho kitakuwa kinatoa huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo nchini humo.
“Ndugu zetu watanzania wapo mbele yetu katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwasababu yatari wameshafungua Taasisi ambayo inatoa huduma za moyo na imewekeza wataalamu na vifaa vya kutosha, naamini tukiendelea kupata ujuzi kama huu nasi tutaweza kufungua Hospitali ya Moyo”, amesema Khumbize
Khumbize amesema matibabu ya moyo ni ya gharama, hadi sasa Malawi ina wagonjwa zaidi ya mia tano wenye magonjwa mbalimbali ya moyo wanaosubiria kuwapeleka nje ya Malawi kwa ajili ya matibabu.
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka (JKCI) Parvina Kazaura, amesema katika kambi hiyo walifanya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watu wazima na watoto ambapo kila siku watoto zaidi ya 80 wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi wa moyo na kubaini watoto wengi walikuwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo na wachache kuwa na magonjwa ya moyo waliyoyapata wakati wa ukuaji.
“Kwa bahati mbaya watoto wengi wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wamekuja wakiwa na umri mkubwa ambapo ilipaswa kufanyiwa upasuaji mapema baada ya kuzaliwa lakini hawakufanyiwa kutokana na huduma hizi kutokuwepo hapa Malawi,”amesema.
Dk. Parvina amesema watoto ambao kutokana na umri wao kupita wakati wa kufanyiwa upasuaji wa moyo wameangalia matibabu wanayoendelea kuyapata na kuwashauri wataalam wa afya wanaowahudumia ni dawa gani wanapaswa kuzitumia ili waweze kuwa sawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo Nchini Malawi Dk. Chimota Phiri, amesema kambi ya matibabu ya moyo iliyofanywa na wenzao kutoka JKCI imewapa mwanga wa kuyatambua magonjwa mbalimbali ya moyo waliyonayo wananchi wa Malawi
“Nchi yetu sasa inatakiwa kuwekeza katika taaluma ya kibingwa ya matibabu ya moyo ili wataalam wetu waweze kwenda kujifunza na kuwasaidia wananchi wetu kupata huduma hapa nchini badala ya kuanza kuhangaika kutafuta huduma za matibabu ya moyo nchi za mbali”, amesema Chimota
Lay Pastor Kachoka mwananchi wa Malawi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo amewashukuru madaktari kutoka JKCI kwa kumfanyia uchunguzi wa kina na kumshauri kuhudhuria kliniki ya matibabu ya moyo kila baada ya miezi sita.
“Sisi wananchi wa Malawi tunahitaji sana huduma hizi kuwepo hapa nchini kwetu, nawashauri wakati mwingine watakapoandaa kambi kama hii waweke maeneo tofauti tofauti ya nchi yetu ili wananchi wote waweze kufaidika na huduma hizi”, amesema Lay Postor.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi