November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko: Rais Samia amewaunganisha watanzania,asisitiza malezi bora

Na Mwandishi wetu Timesmajira online,Chemba

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaunganisha watanzania katika Sekta zote nchini ili kuhakikisha wananufaika na rasilimali mbalimbali zilizopo pamoja na kujenga uchumi wa Taifa.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa kutoka Jumuiya ya Wazazi katika Maadhimisho Wiki ya Wazazi Kimkoa (Miaka 68 ya Jumuiya) yaliyofanyika jana wilaya ya Chemba kwa Mtoro, Mkoani Dodoma

“Rais Samia na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi amefanya kazi kubwa ya kuwaunganisha watanzania, leo wote tunaimba maendeleo, wote tunaimba maji, wote tunaimba barabara,  wote tunaimba madarasa kwa ajili ya watoto wetu na wote tunaimba maendeleo kwa ajili ya nchi yetu,” amesema Dkt. Biteko.

Akizungumzia kuhusu shule ya Sekondari Kuryo iliyosimana kwa muda mrefu amesisitiza kuwa atasimamia ili uvumbuzi upatikane na hatimaye shule hiyo ianze kufundisha. Pia, amewataka wananchi wa wilaya ya Chemba kuungana kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameitaka Jumuiya ya Wazazi wa wilaya ya chemba na Taifa kuwekeza kwa wototo ili Taifa liweze kufanikiwa kwa kuwapatia elimu na kuwafundisha malezi yaliyo bora na kuwa kizazi chenye maadili.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa Samwel Malecela amemshukuru Dkt. Doto Biteko kwa kukubali  kuwa Mgeni rasmi maadhimisho hayo. Amesisitiza wananchi kupendana na kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu taratibu za nchi zilizowekwa.

Dkt. Biteko ametembelea eneo la Shule ya Sekondari Kuryo na kufungua Shina la wakereketwa. Kauli Mbiu ya maadhimisho hayo ni “Taifa Bora, hutokana na Malezi Bora ya Watoto”. Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa, Mbunge wa Jimbo la Chemba Mohamed Monni na wananchi wa wilaya hiyo.