November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 1.5 kujenga miundombinu shule za msingi Ilemela

Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela imepokea kiasi cha zaidi ya bilioni 1.57,kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule 7 za msingi na awali kupitia mradi wa Boost zilizopo katika halamashauri hiyo.

Ambapo utekelezwaji wa mradi wa Boost unatarajia kuboresha kiwango cha elimu na fursa za upatikanaji wa elimu kwa watoto wa elimu ya awali na msingi Tanzania Bara.

Sambambamba na uboreshaji wa miundombinu, kuinua ubora wa walimu wa shule za awali na msingi na usimamizi na utawala bora katika utoaji huduma ya elimu.

Ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inayotoa tamko kuwa Serikali itahakikisha kuwepo kwa miundombinu bora na stahiki ya kutosheleza mahitaji ya elimu na mafunzo kwa makundi yote katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ,Halmashauri ya Ilemela Violencea Mbakile,iliyotolewa Aprili 27,2023.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa halmashauri hiyo imepokea fedha hizo kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule hizo kupitia mradi huo.

Ambapo kati ya fedha hizo bilioni 1.08,zitatumika kujenga shule mbili mpya za msingi zenye mikondo miwili,milioni 400 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 16 katika shule nne za msingi.

Huku milioni 69.1 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya mfano elimu ya awali na milioni 25.2 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule nne za msingi.

Hata hivyo shule za msingi ambazo zimepokea fedha hizo ni pamoja na shule ya Buswelu ,Chasubi, Igombe, Kahama, Nyamadoke,Nyamhongolo na Nyamwilolelwa.