November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msigwa:ripoti ya CAG kufanyiwa kazi

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online,Dodoma

SERIKALI imesema kuwa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inatumika kama nyenzo ili kuhakikisha yale mapungufu yote yaliyobainika yanafanyiwa kazi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Hayo yamebainishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma iliyoambatana na Iftar ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Amesema kufuatia ripoti ya CAG,mapungufu yote yatafanyiwa kazi ili kukomesha vitendo vya ubadhilifu wa fedha.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa akizungumza katika kikao cha waandishi wa habari jijini Dodoma kilichoambatana na Iftar ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Pia ripoti hiyo inatumika kama nyenzo kwa serikali ili kuhakikisha yale mapungufu yote yaliyobainika yanafanyiwa kazi kwa maslahi mapana ya taifa.

Msigwa amesema kuwa serikali ipo kazini na hakuna mradi wowote uliosimama au utakaosimama kwa sababu yeyote ile hivyo miradi ya maendeleo inazidi kuchanja mbuga.

“Niwatoe hofu wananchi, ripoti ya CAG ni nyenzo inayotumiwa na serikali kusimamia rasilimali za Watanzania,hivyo niwahakikishie kupitia ripoti hiyo serikali ipo macho kulinda na kutetea rasilimali,achaneni na taarifa za mitandaoni zinazokatisha tamaa,”amesema Msigwa.

Hata hivyo Msigwa amewata wananchi kuachana na mijadala ya ripoti hiyo ambayo imejaa upotoshaji na isiyojenga yenye lengo la kuharibu taswira ya nchi na badala yake wajikite kwenye ujenzi wa taifa .

Kuhusu miradi ya kimkakati Msigwa amesema mwendo ni uleule hakuna kilichobadilika wala kusimama na kutolea mfano mradi wa reli Morogoro -Makutopora kuwa unaendelea kutekelezwa ukiwa umefikia asilimia 93.3.

“Miradi yote ya kimkakati inaendelea kutekelezwa,serikali ya Rais Samia ina nia ya dhati na itahakikisha mipango yote inatekelezwa ikiwemo mabehewa ya ghorofa,mradi wa uzio wa tembo ambao umeanza kwa mara ya kwanza nchini na barabara ya mzungu ya Dodoma ambayo imefikia asilimia 18.

Baadhi ya waandishi wa habari jijini Dodoma,wakimskiliza Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa hayupo pichani wakati wa kikao naye kilichoambatana na Iftar ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Aidha Msigwa amewataka waandishi wa habari kuendelea na kazi zao bila wasiwasi kwani serikali ya awamu ya sita inatambua, inathamini na itaendelea kusimamia uhuru wa vyombo vya habari.

“Chapeni kazi kwa kuzingatia sheria penye changamoto tushirikishane ili tuweze kuzitatua na jueni tu serikali inatambua sana kazi zenu,”amesema Msigwa.

Kwa upande wao waandishi wa Habari wakiwemo Sylivesta Ngombaniza , Moreen Rojas na Salehe Lujuo kwa nyakati tofauti walimpongeza msemaji huyo kwa moyo wa upendo juu ya waandishi wa habari.

“Tuchukue fursa hii kukushukuru msemaji kwa uzalendo wako hasa sisi waandishi wa Habari umekuwa nasi bega kwa bega kutushauri,kututia moyo,na una mipango mingi mizuri juu yetu na wengine waige mfano wako Mungu akubariki sana,”amesema Ngombaniza.