November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATCL,KQ kushirikiana usafirishaji mizigo

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

KAMPUNI ya Ndege Kenya (KQ) kuingia makubaliano na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa lengo la kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni hizo.

Mtendaji Mkuu wa KQ Allan Kilavuka amesema hayo wakati wa kikao cha awali na viongozi wa ATCL akiwemo Mtendaji Mkuu Mhandisi Ladislaus Matindi.

Akifafanua kwenye kikao hicho, Kilavuka amesema wamelazimika kufanya hivyo kutokana na uwepo wa maeneo mengi ambayo Kampuni hizo zinaweza kushirikiana ikiwemo eneo la usafirishaji mizigo.

Ameeleza kuwa Kenya ni kituo cha usafirishaji mizigo katika bara la Afrika kwa mizigo waliyonayo wanaweza kuingia makubaliano na Tanzania kuhakikisha ndege ya mizigo Boeing 767-300 yenye uwezo wa kubeba tani 54 kwa mara moja, inatumika kikamilifu.

“Hivi karibuni Tanzania itapokea ndege yake ya mizigo ambayo itaweza kutatua changamoto ya usafirishaji mizigo kwa kiwango kikubwa. Sisi tunaamini tunaweza kushirikiana kwenye eneo hili”, amesema Kilavula.

Ameongeza kuwa kwa upande wa abiria, Kampuni hizi zinaweza kushirikiana katika kusafirisha abiria kwa kuzingatia misingi yenye kunufaisha pande zote mbili.

“Kupitia ndege tulizonazo, vifaa na wataalamu wetu wakitumika ipasavyo tutaongeza thamani na kupunguza gharama za uendeshaji wa ATCL na KQ. Uwepo wa ndege ya Boeing 787- 8 (Dreamliner) na ujio wa ndege ya mizigo Boeing 767- 300F zinafungua fursa zaidi za kibiashara, alihitimisha Kilavula.

Naye Mhandisi Matindi amesema kikao hiki kimeangalia masuala yatakayosaidia ustawi wa Kampuni hizi za ndege pamoja na nchi zao kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya soko duniani.

Ametaja maeneo yanayokusudiwa kushirikiana ni pamoja na kubadilishana wataalamu, kuendesha mafunzo kwa vitendo pasipo kutegemea nchi za mbali na usafirishaji wa mizigo, ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni hizi.

“Soko la Afrika peke yake ni kubwa sana na linahitaji ushirikiano katika kulifikia hususani huduma ya kusafirisha abiria na mizigo. Mahitaji mengine ni pamoja na mafunzo kwa vitendo suala linalolazimu kusafirisha wataalamu kwenda nchi za Ulaya kwa ajili ya mafunzo ya siku mbili au tatu.

Iwapo elimu hii inaweza kupatikana nchi jirani, itakuwa bora zaidi ili kuinua uwezo wa kampuni hizo mbili na kuleta tija zaidi kwa jamii inayowazunguka” amefafanua Mhandisi Matindi.

Mhandisi Matindi ametumia nafasi hii pia kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua fursa za biashara na uwekezaji nchini baada ya ziara yake nchini Kenya.

Ziara ya Mtendaji Mkuu wa KQ imepokelewa na mwamko mpya na watendaji wa ATCL ambao wanakiri ni ishara nzuri ya kuwepo mahusiano bora ya kibiashara, kiuchumi na kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili hususan kwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.