Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amewataka wataalamu na watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mji wa Korogwe (KUWASA) kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi, huku akiweka msisitizo hataki takwimu za kupika za upatikanaji maji.
Aweso ametoa agizo hilo Aprili 16, 2023 wakati alipofanya ziara ya siku moja kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga ili kukagua miradi ya maji, na kuzungumza na warumishi na viongozi wa Wilaya ya Korogwe.
“Ninachotaka kuona ni wananchi wa Mji wa Korogwe wanapata maji. Mimi niliwahi kukataa takwimu za kupika. Niliwahi kuja Korogwe, na kusomewa taarifa kuwa wananchi wa Mji wa Korogwe wanapata maji kwa asilimia 80, mimi nikasema hapana.
“Hivyo nataka viongozi na wataalamu mshirikiane ili kuona changamoto za maji kwenye Mji wa Korogwe zinapungua kama sio kuondoka kabisa. Korogwe sio ya kulalamikia vyanzo vya maji wakati kuna Mto Pangani. Nataka unafuu wa upatikanaji wa maji uonekane kwa wananchi, na sio kwenye takwimu” alisema Aweso.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA Sifael Masawa akitoa taarifa ya upatikanaji maji hadi Machi, mwaka huu, alisema wanahitaji sh. 825,334,492 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji iliyopo, ambapo fedha za uchimbaji visima saba ni sh. 230,185,000.
Fedha kwa ajili ya ufungaji wa transfoma Kilole na Old Korogwe, na umaliziaji wa mradi wa Lwengera- Relini na Lwengera- Darajani sh. milioni 110.6, na fedha kwa ajili ya ununuzi wa pampu, mabomba, na ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house) kwa ajili ya visima vilivyochimbwa ili viweze kufanya kazi ni sh. 484,549,092
Masawa alisema changamoto zilizopo ni pamoja na vyanzo vilivyopo vinatosheleza mahitaji ya maji kwa asilimia 70.28. Pia uchakavu wa miundombinu na ukame wa muda mrefu, umeathiri wingi wa maji toka chanzo cha Mto Mbeza.
“Umeme kuwa mdogo na hivyo kufanya pampu kutofanya kazi mchana katika vyanzo vya Mto Pangani eneo la Mtonga na Old Korogwe, na visima vitano vilivyopo, hivyo kufanya uzalishaji kuwa asilimia 52.2 katika vyanzo hivi. Pia ukosefu wa miundombinu ya kusafisha maji, hivyo kufanya maji yanayozalishwa kutokuwa na ubora hasa nyakati za mvua” alisema Masawa.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo, alimuhakikishia Waziri wa Maji kuwa watasimamia kuona shughuli zote zinakwenda kama zilivyopangwa ili wananchi wanapata maji, kwani Serikali inatoa fedha nyingi kwenye Sekta ya Maji kwa ajili ya kuondoa changamoto za maji kwa wananchi.
Aweso ameahidi kuwa wizara itatoa fedha hiyo hiyo sh. 825,334,492 ili kuondoa changamoto ya maji katika Mji wa Korogwe.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria