November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shada la maua la Makamu wa Rais wa Marekani lageuka kivutio makumbusho ya Taifa

Na Mwandishi Wetu

SHADA la maua lililowekwa na MAKAMU WA RAIS wa Marekani,Kamala Harris kwenye onesho maalum la kuwakumbuka wahanga wa Bomu la Ubalozi wa Marekani mwaka 1998 lililopo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam, limewavutia wengi na kufanya wageni wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea Makumbusho hiyo kwenda kupiga nalo picha.

Akizungumzia mafanikio ya ziara hiyo ndani ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa nchini, Dkt. Noel Lwoga, amesema licha ya Taasisi hiyo kutangazika Kimataifa, imeweza kuvuta watanzania wengi kuitembelea Makumbusho hiyo huku wengi wao wakivutiwa na shada la Maua lililowekwa na Kiongozi huyo mkubwa kutoka kwenye Taifa la Marekani.

Dkt. Lwoga ameongeza kuwa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani kuitembelea Makumbusho ya Taifa hasa onesho maalumu la masalia ya Mlipuko wa Bomu kwenye Ubalozi wa Marekani uliotokea mwaka 1998, ni matokeo chanya ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Diplomasia ya Kimataifa.

Hii ni alama kubwa katika kukuza utalii wetu ndani na nje ya nchi na hasa kwa maonesho haya muhimu ya kihistoria ambayo yanaonesha utajiri mkubwa ambao nchi yetu imeuhifadhi lakini hasa historia inayoakisi amani na upendo katika mataifa yetu”. Ameongeza Dkt. Lwoga.

Naye Mkazi wa Kilosa Morogoro Aloyce Adrian aliyefika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kujifunza mambo mbalimbali ya Historia na Utamaduni, amesema baada ya kufika Jijini Dar es Salaam ameamua Kwenda kwenye Makumbusho hiyo ili kuona alichokiona Makamu huyo wa Rais wa Marekani, kutazama na kupiga picha kama kumbukumbu muhimu ya ziara ya kiongozi huyo wa Marekani.

Aidha, ukiachana na kiingilizo kidogo katika Makumbusho hayo, wageni hawa pia wameweza kujionea, kujifunza na kufurahia vivutio vingine vingi kama vile fuvu la zamadamu maarufu kama Zinj lenye miaka milioni 1.7 iliyopita, vitu halisi vya kimila na kitamaduni vilivyotumiwa na mababu zetu, vitu vya kihistoria ikiwemo Hati ya Uhuru wa Tanzania.