November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya Msichana Initiative inavyowakomboa wasichana

Na Penina Malundo

CHANGAMOTO ya wasichana kutembea umbali mrefu kwenda shule,ni moja ya tatizo inayochangia kupata hatari ya matukio ya ukatili wa kijinsia katika kundi hilo na kupelekea kupoteza ndoto zao.

Wasichana wamekuwa wakikubwa na madhira mbalimbali ikiwemo Mimba za utotoni,uchelewaji wa masomo shuleni kutokana na umbali kati ya shule na nyumbani hivyo kusababisha kukosa masoma kwa wakati.Watoto wa kike ndio wahanga wakubwa wanaokumbwa na changamoto mbalimbali katika kupata elimu bora, ambapo changamoto wanazokumbana nazo huvuruga mfumo mzima wa maisha ya watoto wakike na kusababisha kushindwa kutimiza zao.

Licha ya vikwazo wanavyopitia katika kupata elimu bora, wasichana wamekua wakipitia matukio ya ukatili wa kijinsia kama vile kubakwa,kuozeshwa katika umri mdogo, mimba za utotoni na wengine kuacha shule kabisa kutokana na kutembea umbali mrefu wakati wa kuelekea na kurudi kutoka shule hasa kwa wasichana wanaosoma shule za umma za Msingi na Sekondari. Ripoti mbalimbali zinaonyesha shule nyingi za sekondari zilizopo maeneo ya Vijijini huwaladhimu wasichana kutembea umbali kuanzia km nne hadi 10 kwenda na kurudi kutoka shule ambapo husababisha wasichana kukutana na matukio hayo ya ukatili wanapokuwa njiani.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu,ustawi wa jamii na mashirika ya kitaifa na kimataifa yamekuwa yakipiga kelele juu ya kutafuta njia ya kupunguza hali ya wasichana kutopata unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo kupata mimba za utotoni na kupata haki ya elimu kama wapatavyo watoto wengine.

Miongoni mwa wadau hao ni pamoja na Shirika la Msichana Initiative kupitia mradi wake wa Baiskeli Moja kwa Msichana Mmoja limeendelea kugusa wasichana wenye changamoto hizo na wameweza kuwafikia wasichana 50 kwa shule ya Sekondari Babayu na Zanka zilizopo Wilaya ya Bahi ,Dodoma. Katika zoezi la ugawaji Baiskeli lilofanyika katika mikoa ya Dodoma,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi anawasisitiza wanafunzi kujiamini na kujitambua wanapokuwa shuleni na kuhakikisha wasoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao.

Anasema Msichana Initiative imekua ikitekeleza mradi wa “BAISKELI MOJA, MSICHANA MMOJA’’(ONE GIRL ONE BIKE) toka mwaka 2017, wenye lengo la kusaidia wasichana wanaotembea umbali zaidi ya kilomita 10 kwenda na kurudi kutoka shule.Gyumi anasema mradi huo unalengo la kusaidia kutatua changamoto ya kupunguza hatari ya matukio ya ukatili kwa wasichana.

”Kama Shirika mpaka sasa tumefanikiwa kugawa zaidi ya Baiskeli 548 tangu kuanza kwa mradi huu mwaka 2017,tunawashukuru sana washirika wetu Malala Fund,wamejitoa kwa hali na mali katika kuwasaidia wasichana wa Tanzania kufikia ndoto zao za kielimu,”anasema.Makamu wa Shule ya Sekondari Babayu,Steve Kimbwili anasema mradi huu umekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa shule hiyo katika kubadilisha maisha ya wanafunzi wanapokuwa wanasoma.

”Kwa kweli tunashukuru Malala Fund kwa kujitoa kwa wanafunzi hawa na kuja kutusaidia kutoa msaada wa baskeli 25 kwa wasichana wa shule yetu kwani ni watoto ambao wanaotoka mbali na mazingira ya shule,”anasema.

Anasema wapo wanafunzi wa shule hiyo ambao wanaotoka mbali zaidi ya kilometa tano na wengine kilometa 10 ,ambapo katika shule hiyo takwimu zinaonyesha kuwa takribaini zaidi watoto 50 wa shule hiyo wameacha shule mwaka 2022 kati yao Wasichana wakiwa 32 na Wavulana wakiwa 18.Kimbwili anasema sababu ya watoto hao kuacha shule ni pamoja na changamoto ya umbali ambapo wanafunzi wanakata tamaa ya masomo pindi wanapotembea umbali mrefu kutoka majumbani mwao.

”Ujio huu wa Malala Fund utasaidia kupunguza changamoto kwasababu watoto hao watakuwa wamefarijika na kuona jitihada zinazofanyika kuhakikisha kwamba licha ya umbali wao wanaweza wakapata elimu stahiki na hatimaye kufikia ndoto zao,”anasema na kuongeza

”Tunashukuru sana Malala Fund kwa hatua hii,tunaomba kuongeza baskeli nyingine kwani hizi bado hazitoshi ili kuleta faraja kwa watoto,watoto hawa wanatoka mbali kwaajili ya kufika shuleni na kuendelea na masomo,”anasema.

Anasema taasisi hiyo imeibua ndoto za watoto wa kike hasa wasichana wanaotoka mbali zaidi kufika mahala ambayo kila mtu amekuwa anatamani kuendelea na shule kwani anaona hata kama anatoka mbali anaweza akapata usafiri na kuendelea na masomo.

”Msaada huu umeleta chachu kubwa sana na hamasa ya kuona wanawasaidia watoto hawa waweza kupata elimu bila kujali umbali fulani, ninawaasa wanafunzi wajitahidi sana kuzitunza baskeli walizopata waweze kuwasaidia ili kuhakikisha kila siku wanakuja shuleni kwa ufaulu wao kwani hii italeta hamasa katika mashirika mengine kuleta msaada,”anasema.

Anasisitiza Wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuweza kufikia ndoto zao”Nashuruku kwa ujio wa Msichana Initiative kuja kutufikia na kuweza kutoa misaada ya baskeli 25 kimsingi ni msaada mkubwa sana tangu shule imeanzishwa mwaka 2007 hakuna kampuni au shirika lililofikilia kuna suala la watoto wanaotoka mbali ambao wanakutana na changamoto nyingi sana ikiwemo kupata ujauzito kuacha shule na vitu vingine,”anasema.

Kwa Upande wake Sophia Mnubi,Mwalimu wa Taalamu wa shule hiyo ya Babayi anasema msaada huu wa baskeli kwa wanafunzi wa kike wanaotoka katika mazingira ya mbali ni msaada mkubwa sana kwao katika hali ya kitaaluma,usalama njiani wakiwa wanatoka nyumbani na kuja shuleni ,kuokoa muda mambo ya kifamilia anapokuwa shuleni.Anasema kwa upande wa kitaaluma,msaada huo utawasaidia wanafunzi hao kuwahi vipindi vya asubuhi na vile vya darasani vinavyoanza saa mbili asubuhi na kuwasiadia kuwainu katika kiwango cha taaluma katika masomo yao.

”Huu msaada kwa watoto hawa wakike utawasadia kushinda vishawishi vya njiani ,kwani mtoto anapotembea kwa miguu kutoka nyumbani kuja shuleni anakutana na vishawishi vingi njiani hususani kwa vijana wakiume hivyo kwa kutumia baskeli itasaidia kwa kiasi kikubwa kuepukana na changamoto hizo,”anasema.

Amina Kamau ni Mmoja wa Wazazi ambaye mtoto wake amenufaika na mradi huo,anasema msaada huo wa baskeli ni msaada mkubwa kwake kwani itamsaidia mwanae kwa kiasi kikubwa kusoma vizuri bila kukumbana na changamoto yoyote.Mama Amina anasema mwanae amekuwa akiamka alfajili ya saa 11 na nusu na kutembea umbali mkubwa kilometa 10 kwenda shuleni kwao ambapo wakati mwingine anakuta masomo yameanza na kumfanya kuchelewa.

Pia anasema msaada huo, utamsaidia mwanae kuepukana na majanga mbalimbali ya njiani kama ubakaji, na vishawishi vya njiani .”Nashukuru kwa msaada wa baskeli alikuwa anatembea umbali wa muda mrefu ..kwa sasa hivi atatumia muda mchache wa kufika shuleni na kuwahi masomo kama wenzake wanaoishi karibu,”anasema.

Axcese Songo Mwanafunzi Darasa la Kidato Pili Shule ya Sekondaro Babayi ,anashukuru Shirika la Msichana Initiative kwa kuwapa msaada wa huo wa Baskeli na kuhaidi kuwahi na kutimiza ndoto zangu.