November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAC yaeleza Serikali ya awamu ya sita ilivyoboresha Sekta ya usafiri majini kupitia shirika hilo

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)umeeleza juhudi za Serikali ya awamu ya sita ilivyoboresha Sekta ya usafiri majini ikiwemo kuunda nyenzo za udhibiti wa huduma za usafiri kwa njia ya maji.

Hii ni pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali ambapo jumla ya kanuni mpya 11 chini ya Sheria ya Uwakala wa Meli, Sura 415 na kanuni nyingine 32 chini ya Sheria ya Usafiri Majini, Sura 165 zimeshaandaliwa na kuanza kutumika.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 7,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Mkeyenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na utekelezaji wa shughuli za shirika hilo,ambapo alisema Kanuni hizo zimeimarisha na kuboresha kwa kiasi kikubwa usimamizi wa sekta ya usafiri majini na zimeendelea kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili ziwafikie wadau wengi ili kufikia lengo lililokusudiwa katika utunzi wa Kanuni hizo.

Mkeyenge ametaja mafanikio mengine kuwa ni Kuwashirikisha wadau katika maamuzi ya kiudhibiti na masuala mengine yanayowahusu ili kuimarisha mahusiano.

Mafanikio mengine ni kuwezesha ongezeko la idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa na TASAC ambapo idadi ya leseni na vyeti vya usajili ilifikia 1,195 kwa mwaka wa fedha 2021/22 ikilinganishwa na leseni na vyeti vya usajili 941 katika mwaka wa fedha 2018/19 sawa na ongezeko la asilimia 79.

“TASAC imewezesha ongezeko la idadi ya vyeti vya mabaharia waliokidhi masharti kutoka 6,068 katika mwaka 2018/19 hadi kufikia 19,575 katika mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 31,”amesema Mkeyenge.

Aidha Mkeyenge amesema TASAC imeweza kuimarisha usimamizi wa usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira dhidi ya shughuli za meli ili kupunguza matukio ya ajali za vyombo vya majini ambapo kaguzi za vyombo vya usafiri majini zilifanyika 6,208 katika mwaka wa fedha 2021/22 na kaguzi 4,490 katika kipindi cha  Julai 2022 mpaka Januari 2023 inayotarajiwa kufikia vyombo takriban 8,000 ifikapo mwezi Juni 2023.

Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo ametaja am fursa zinazopatikana katika sekta ya usafiri majini ambazo zinaweza kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi ni pamoja na  kuanzisha utaratibu wa kusajili meli kwa masharti nafuu (open registry).

Ametaja fursa nyingine kuwa ni kuanzisha maeneo ya ukarabati na ujenzi wa meli katika ukanda wa pwani, kuanzisha maegesho ya boti ndogo katika ukanda wa pwani, kuanzisha viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki na kujenga bandari rasmi za uvuvi.