December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bangu:Madalali waacheni wakulima watumie mfumo wa stakabadhi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline, Dodoma

BODI ya usimamizi wa Stakabadhi za ghala (WRRB)imesema kumekuwepo na vitendo vya ulanguzi wa ununuaji mazao kinyume na mfumo wa Stakabadhi hivyo imewataka  madalali wote wanaofanya vitendo hivyo  kuacha tabia hiyo.

Hayo yasemwa jijini hapa leo,Februari 15,2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Asangye Bangu ,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za bodi hiyo ambapo amewataka madalali hao kuacha kuwarubuni wakulima na badala yake wawaache waingie katika mfumo wa Stakabadhi.

“Kumekuwa na wimbi la watu wanakwenda mashambani kwa wakulima na kuwadalalia mazao wakulima na kununua kwa bei ya chini tofauti kabisa na bei ya mazao yao  kitu ambacho kinaendelea kudidimiza maendeleo ya wakulima,”amesema Bangu.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana toka kuanzishwa kwa mfumo huo wa Stakabadhi za Ghala ni pamoja na ongezeko la  bei za mazao, mapato ya mkulima na mapato ya Serikali kwa wastani wa asilimia 200% kutokana na urasimishaji.

Pia amesema mafanikio mengine ni ,ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 20 kwa mwaka,  kichecheo cha ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni, upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Sambamba na mafanikio hayo amesema kuwa pia kumekuwepo na ongezeko la mapato ya uhakika kwa Serikali Kuu na Serikali Mitaa na   kukuza huduma za fedha vijijini.

Sambamba na hilo amesema kuwa tangu mwaka 2007 hadi sasa kilo bilioni 2.3 za mazao ya nafaka zimepitishwa na bodi hiyo na kilo hizo zinatokama na mazao 11 yanayolimwa hapa nchini.

Hata hivyo Bangu amesema kuwa bodi inashirikiana na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima kwa lengo la kuwafanya wakulima kupata mazao bora na salama ambayo yataweza kuingia katika soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha ameeleza kuwa bodi hiyo kwa sasa imekuwa ikishiriki kupata mazao ambayo hayapo katika bodi ili nayo yaweze kuingizwa katika ghala huku wakiangalia ni jinsi gani ya kuanzisha maghala ya mazao ya kuoza kama vile maparachichi na nyanya pamoja na mazao mengine.

Ukiachana na mazao hayo ameeleza kuwa kwa sasa bodi inafikilia na ipo katika mazungumzo na wizara ya mifugo ili kuweza kuanzisha maghala ya mifugo kama vile ngozi sambamba na mazao ya nyuki .

Hata hivyo amezitaja changamoto kadhaa kuwa ni pamoja na kukosekana kwa elimu juu ya mfumo ambao unatumiwa na bodi hiyo kwa kuwepo na maneno ya uzushi juu ya mfumo huo.