November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBA yatekeleza agizo la Rais nyumba za magomeni kota

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umesema umetekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhusu kupunguza bei za nyumba za Magomeni Kota,jijini Dar es Salaam.

Hayo  yameelezwa jijini hapa leo ,Februari 14,2023,na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo,Daud Kondoro wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  utekelezaji wa majukumu ya Wakala huo kwa mwaka 2022-2023.

Kondoro ameeleza kuwa  baada ya maagizo ya Rais walikutana na timu ya watalaamu na kujadiliana namna ya kunguza bei ya nyumba hizo.

Ambapo amesema kutokana na maelekezo ya Rais wameweza kuondoa shilingi bilioni 18.2 na kwa sasa bei ya nyumba ya chumba kimoja itauzwa  kutoka Shilingi  Milioni 74.8  hadi Shilingi milioni 48 na ya  nyumba viwili kutoka Shilingi milioni 86 hadi Shilingi milini 56.9.

“Hii ni kutokana na kupunguza bei ya nyumba hizi kwa  kuondoa gharama za ardhi,maeneo jumuishi kama korido, mandhari ya nje,mashimo ya maji taka na  vizimba vya taka ngumu vilivyokuwa vimejumuishwa awali,”amefafanua

Aidha amesema timu imekubaliana deni litarudishwa kwa miaka 15 na miaka mitano watakaa bure lakini hakutakuwa na riba.

“Niseme hakuna sakata kwa upande wa wakala tunatambua umoja wa wanakota,”amesisitiza.

Machi 23 mwaka jana Rais Samia wakati akizindua nyumba hizo aliutaka   Wakala huo kupunguza gharama za uuzaji wa nyumba hizo kwani zipo juu.

Awali nyumba hizo zilikuwa zikiuzwa kwa  Sh74 milioni kwa chumba na sebule  na Sh86 milioni kwa vyumba viwili na sebule.

Februari 6 mwaka huu wakazi 644 wa Magomeni Kota waligomea  kusaini mkataba wa kuanza kununua nyumba hizo, kwa madai kwamba bei waliyoletewa sio rafiki na haiendani na hali ya uchumi wao.

Akizungumzia utekeleza wa majukumu ya TBA kwa mwaka  2021/22 2022/23 Kondoro ametaja miradi iliyotekelezwa kwa fedha za ruzuku  amesema kuwa 

 TBA ilipokea jumla ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 54.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi yake ikiwemo

Mradi wa Ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni Dodoma.

Ametaja miradi mingine ni mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za viongozi jijini Dodoma,Ujenzi wa nyumba za Watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni Kota, awamu ya kwanza na ya pili,Ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Temeke Kota ambapo linajengwa jengo la ghorofa 9 linalochukua familia 144.

“Umaliziaji wa ujenzi wa nyumba tano za majaji katika mikoa ya Tabora, Kilimanjaro, Mtwara, Kagera na Shinyanga,  ambapo nyumba nne zimeshakamilika na kuanza kutumika,Ujenzi wa nyumba ya jaji Kagera unaendelea na umefika 30% ya utekelezaji huku Ukarabati wa nyumba 40 za viongozi jijini Dodoma, awamu ya kwanza na ya pili, Ukarabati wa nyumba 30 jijini Dar es Salaam,Ukarabati wa nyumba 66 za iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), pamoja na Ukarabati wa nyumba katika Mikoa 20 zilizohamishiwa TBA kutoka TAMISEMI.