November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ndalichako  aipongeza PSSSF kwa kutekeleza agizo la Rais

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Morogoro

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu),  Prof. Joyce Ndalichako, amepongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt.Samia Suluhu Hassan la kulipa wastaafu mafao kwa wakati.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (aliyesimama) akizungumza wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye ukumbi WA Magadu mjini Morogoro Februari 2, 2023. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba na kulia ni Katibu wa Baraza, Steven Biko.

Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo mjini Morogoro alipokuwa akizindua Baraza la pili la wafanyakazi wa mfuko wa PSSSF.

“Mlitumie baraza hili kuhimiza kila mfanyakazi ajue wajibu wake ili kuuwezesha mfuko kusonga mbele katika kutekeleza maagizo ya serikali pamoja na kutoa huduma bora kwa wanachama,”amesema.

Aidha, amesema rais ameendelea kushughulikia changamoto za wastaafu ikiwa ni pamoja na kuwataka watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii kulipa mafao watumishi walioondolewa kazini kwa kubainika kuwa na  vyeti feki.

“Kulikuwa na jumla ya watumishi Elfu Kumi na Nne (14,000) ambao waliondolewa kwenye utumishi kwa sababu ya vyeti feki, tayari watumishi 6,892 wameshalipwa na 3,169 bado madai yao yanafanyiwa kazi,” alifafanua.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PSSSF, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu, CPA Hosea Kashimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa baraza hilo

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, amesema kwasasa mafao hayo ya wastaafu wanalipwa ndani ya siku 60 na uhakiki wa wastaafu unafanyika kidigitali.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mfuko kwa nusu mwaka toka Julai 2022 hadi Desemba 2022, CPA Kashimba alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa aliyofanya ya kuhakikisha watanzania wengi wanapata ajira.

“Tumevuka lengo la kuandikisha wanachama kwa asilimia 270%, lengo letu lilikuwa kuandikisha wanachama 13,000, lakini tumevuka lengo hilo na kuandikisha wanachama 33,534, sisi wanachama wetu wanategemea jinsi serikali inavyoajiri, watu wengi wameajiriwa katika kipindi hicho.” Alisema.

Eneo lingine ambalo Mfuko umefanya vizuri ni makusanyo ya Michango ambapo lengo lilikuwa ni kukusanya Shilingi Bilioni 792 lakini Mfuko umeweza kukusanya Shilingi Bilioni 823 na hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 104%.

Kuhusu mapato yatokanayo na uwekezaji unaotokana na vitega uchumi, CPA Kashimba alisema Mfuko uliweka lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 256 na badala yake Mfuko umeweza kukusanya Shilingi Bilioni 297 na hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 116%.

Baraza hilo linalofanyika kwa siku mbili, limechagua viongozi wapya wakiwemo Katibu wa Baraza Bw. Steven Biko na Katibu Msaidizi Linda Njoolay.