October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka

Dkt. Mwinuka amtaka Mkandarasi kuongeza kasi ujenzi Ofisi za TANESCO Geita

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka, amewataka Wakala wa Majengo (TBA) kuongeza kasi ya ujenzi wa ofisi za TANESCO Mkoa wa Geita pamoja na Wilaya ya Chato.

Dkt. Mwinuka ametoa agizo hilo alipotembelea na kukagua ujenzi huo akiwa ameambatana na Menejimenti ya TANESCO

Amesema, ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya jitihada za TANESCO kuhakikisha inaendesha shughuli zake katika majengo yake na ili kuepukana na gharama kubwa za upangishaji kuanzia ngazi za Kanda, Mkoa mpaka Wilaya.

Amesema, lengo hilo linakwenda sambamba na maagizo ya serikali ya kuhakikisha kuwa ofisi zote za serikali na umma zinajenga na kumiliki majengo ya ofisi zake katika maeneo yote ambapo zinaendesha shughuli zake.

“Leo nimetembelea kukagua na kujionea ujenzi unaoendelea wa majengo ya ofisi za TANESCO Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato, ambapo yote ujenzi wake unakwenda vizuri chini ya Mkandarasi TBA akiwa chini ya usimamizi wa karibu wa TANESCO, niwaagize kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha majengo haya mapema zaidi ili Shirika liweze kuondokana na matumizi ya nyumba za kupanga kama ofisi na kuhamia katika majengo yak”, amesema Dkt. Mwinuka

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Godfrey Mwakabole amesema, ujenzi unakwenda vizuri na kwa kasi inayoridhisha na matatajio yaliyopo ni kumaliza majengo yote mawili ndani ya mwezi Agost 2020 ili TANESCO iweze kuhamia katika majengo hayo tayari kwa kuendelea Na shughuli zake.

“Ujenzi unakwenda vyema na tunapata ushirikiano mzuri sana kutoka TANESCO katika ujenzi wa majengo haya na niwaahidi kukabidhi majengo bora na kwa wakati, changamoto zilizopo ni ndogo ndogo ambazo huwa tunakaa vikao vya mara kwa mara na Mteja wetu TANESCO na kuzipatia ufumbizi haraka bila kukwamisha utekelezaji wa miradi hii,” amesema Mwakibole.

Kwa upande wa TANESCO Mkoa wa Geita, Meneja wa Mkoa huo Mhandisi Joachim Ruweta ameishukuru Menejimenti ya Shirika kwa ushirikiano mkubwa ambao imekuwa ikiutoa katika kuharakisha shughuli za ujenzi wa majengo hayo na kueleza kuwa, kukamilika mapema kwa majengo hayo itakuwa ni moja ya hatua kubwa katika uboreshaji wa huduma za umeme na mazingira ya kufanyia kazi kwa wafanyakazi wa ofisi husika.