Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online
MKURUGENZi wa Taasisi isiyo ya kiserikali, Pro-Life Tanzania, Emily Hagamu amesema kua mmomonyoko wa maadili ndio chanzo cha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili, unyanyasaji na ulawiti.
Hagamu amesema hayo kwenye mkutano uliofanyika Jijini Dar es salaam Jana ambapo alisema kuwa, wazazi, walezi na viongozi wa dini wameshindwa kutimiza wajibu wao kulingana na nafasi zao, hali iliyosababisha kizazi kilichopo kuendeleza kufanya vitendo hivyo bila ya kuwa na hofu ya Mungu.
Amesema kuwa, katika kipindi cha hivi karibuni, kumekua na taarifa mbalimbali za vitendo hivyo, hali iliyosababisha jamii kuishi kwa hofu huku kila moja kutomuamini mwenzake kutokana na kuendeleza kqa unyanyasaji na ukatili katika jamii zinazowazunguka.
Amesema kuwa, ifike wakati kila moja atimize wajibu wake ili kupunguza vitendo hivyo.
” Sasa hivi wananchi hawaaminiani wenyewe kwa wenyewe katika jamii inayowazunguka, hayo yote yanatokana na ongezeko la vitendo vya ukatili, ulawiti na unyanyasaji, hivyo basi wakati umefika wa kila mmoja kutimiza wajibu wake na kukemea kwa nguvu zote ili visiweze kujitokeza” amesema Hagamu.
Ameongeza kuwa, lakini pia baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa mimba, hali inayosababisha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili.
” Baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa mimba ambacho ni ukatili wa hali ya juu, kwa sababu ni mauaji kama mengine, tunapaswa kukemea vitendo hivyo na kuendelea kuwashauri watoto wetu wasiweze kujihusisha na vitendo hivyo kwa sababu vinaweza kuwaletea madhara iwe ya kiafya au kiakili,” amesema.
Amesema kuwa, wakati umefika kwa viongozi wa dini kukemea vitendo hivyo kwenye madhabahu yao, huku jamii ishirikiane na serikali kukomesha vitendo hivyo na wale watakaobainika wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM