October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga na Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule wakiingia katika viwanja vya TAKUKURU jijini Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa leo. (Picha na Joyce Kaisiki).

Wabunge CHADEMA wavunja ukimya baada ya mahojiano mazito TAKUKURU

Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online,Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalum Suzan Lyimo amesema,katika kukijenga chama lazima kuwe na utaratibu wake,na huo wa kuchangishaba fedha ndio utaratibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hata hivyo, amehoji kwa nini mbunge amekaa miaka 10 ndani ya chama iweje anapoanza kutoka ndipo aseme kuhusu jambo hilo.

“Inakuwaje mbunge amekaa madarakani miaka mitano hadi kumi,utaratibu huo ulikuwepo, lakini miaka yote hiyo hakuwahi kusema ila anapoanza kutoka sasa ndio anasema?amehoji Suzan.

Suzan ambaye ni miongoni mwa wahojiwa,ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma muda mfupi mara baada ya kuhojiwa na TAKUKURU kuhusu matumizi ya fedha ndani ya chama hicho.

Naye Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga amesema,wabunge wanaohama CHADEMA na kwenda vyama vingine waache kuudanganya umma kuhusu makato ya wabunge ambayo yapo kikatiba kwa ajili kukijenga chama.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhojiwa na TAKUKURU leo jijini Dodoma, Haonga amesema,wabunge hao wabakwenda kwenye vyama vingine na kuudanganya umma wakati wanajua suala hilo lipo kikatiba.

“Wabunge hawa wana nia ovu dhidi ya CHADEMA,tunajua wabunge hawa wana nia ovu ya kukisambaratisha chama na ninapenda kuwaambia katika chama tulianza na Mungu na tutamaliza na Mungu.Swali la kujiuliza kwa nini hili liibuke sasa wakati alishasoma katiba na aliielewa ,sasa anapoanza kutoka kwenda vyama vingine ndio anaanza kulalamika,”amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule amesema,makato ya chama yaliyoleta utata yapo katika katiba ya chama hicho Ibara ya 7(a)na 7(b) na kila mbunge alitoa fedha hiyo kwa mujibu wa katiba.

Amesema, fedha hizo ni kwa ajili ya kukijenga chama ambapo mbunge wa jimbo anakatwa asilimia 10 na viti maalun anakatwa asilimia 30 ya mapato yake.