Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Usafirishaji nchini (TSC), Sallu Johnson amesema wanafunzi wanatakiwa kujifunza kwa vitendo ili waelewe namna ya kufanya kazi zao vizuri na kwa weledi.
Johnson amesema hayo leo baada ya kuzindua Tamasha la Taaluma linalojulikana kama ‘Career Fair’ katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa lengo la kuwajengea uwezo na taswira mbalimbali na fursa pia.
Pia, amesema kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa mchango unaonekana kwenye kujenga kizazi chenye weledi kwa sababu hata yeye ni zao la NIT lakini alipotoka chuoni hapo aliweza kupata kazi mbalimbali za Kimataifa.
“Natumaini yangu tukio hili litakuwa ni chachu ya ushirikiano baina ya chuo na sekta mbalimbali ikiwemo ya usafirishaji kwa sababu kampuni zilizoalikwa hapa za umma na binafsi zote zinazohusika moja kwa moja na usafirishaji,”amesema Johnson
Johnson amesema pia, tukio hilo linaakisi dira ya muelekeo wa nchi kwa kuwa na uchumi imara unaojengwa na mifumo imara ya sekta ya usafirishaji kama Taifa, kwa hiyo wanahitaji ushirikiano huo uendelee.
“Nahitaji kuona matokeo ya soko la ajira yanafikiwa kwa kuendelea kuboresha mitaala ya mafunzo chuoni na kupata ushirikiano zaidi kutoka kwa wadau,”amesemaÂ
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema lengo la tamasha hilo pia ni kuwajengea uwezo mkubwa zaidi walimu kujua nini ambacho kinaendelea na pia vijana kuona matakwa ya waajili.
Amesema kuwa kwa namna hiyo wanaamini kuwa hiyo ni sehemu ya ushindi kwa maana kwamba waajili waliyokuwepo hapa wataanza kujua na kuona bidhaa za sasa zikoje.
“Hii itawajengea uwezo na taswira mbalimbali wale wa mwaka wa kwanza watakuwa na miaka miwili ya kujipanga vizuri, wa mwaka wa pili wana mwaka mmoja na wale wa mwaka wa tatu hawajachelewa wanaweza kupata fursa,”amesema Profesa Mganilwa
Profesa Mganilwa amesema tamasha hili litawasaidia kama wakipata kazi waende watumike vipi kwenye nafasi hizo na pia itawasaidia wanafunzi kujiajili wenyewe ndiyo maana wamezialika hadi kampuni binafsi.
Amesema kuwa chuo kwa sasa kina programu nyingi sana na kwa wingi huo wana jumla ya wanafunzi 14,000 kuanzia diploma hadi master’s.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato