November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Gwajima: Ushirikishwaji wa wanaume kupinga ukatili wa kijinsia ni muhimu

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wadau wote duniani kuona umuhimu wa wanaume kushiriki vita dhidi ya ukatili wa kijinsia unaowaathiri zaidi wanawake na watoto.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Wanawake na Haki uliofanyika Jijini Instabul, Uturuki tarehe 5 Novemba, 2022 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Akitoa salaam za Rais Samia, Waziri Dkt. Gwajima ameishukuru Serikali ya Uturuki kwa mwaliko wa mkutano huo wenye Kaulimbiu ya Kanuni za Kimataduni na Wanawake (Cultural Codes and Women), amesema maendeleo ya kijamii na vizazi siyo suala la wanawake tu ni la jamii yote.

Waziri Dkt. Gwajima ameeleza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuwezesha maendeleo yanayozingatia usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili kwa wanawake unaochangiwa na mila na desturi potofu.

Amesema, sambamba na kuendelea kutelekeza makubaliano ya kikanda na kimataifa kuhusu wanawake na maendeleo kuelekea usawa wa kijinsia wanawake wanaendelea kuwezeshwa kwenye elimu, uongozi wa kisiasa, kitaaluma na kijamii.

Amebainisha, uwiano wa uandikishaji wa watoto wa kiume na wa kike shule ya msingi kufikia 1:1 huku Serikali ikitekeleza mpango wa elimu bila ada kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Aidha, mpango wa kujenga Shule moja maalumu ya Sekondari kwa wasichana katika mikoa yote 26 nchini Tanzania kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi, teknolojia, injinia na hesabu kwa kifupi (STEM) jambo ambalo litawainua watoto wa kike kielimu.

Kwa upande wa wanawake na uongozi Waziri Dkt. Gwajima ameueleza mkutano huo kuwa, Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuwainua wanawake. Pamoja na takwa la Katiba ya Nchi kuwa 30% ya viti vya bunge ni viti maalumu kwa ajili ya wanawake na 33.3% ni viti maalumu vya madiwani wanawake, Rais Samia ameongeza idadi ya Mawaziri kamili wanawake hadi 9 huku akiwapa kuongoza Wizara nyeti kwa maendeleo ya Taifa.
Vilevile, Mabalozi Wanawake na Majaji wanawake wameongezeka na ongezeko hilo limeenda sekta zote ngazi zote.

Kuhusu changamoto za mila potofu za ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni, mzigo mkubwa wa majukumu ya wanawake jambo linalozuia wanawake kushiriki shughuli za maendeleo, changamoto za kiuchumi na matukio ya ukatili wa kijinsia Dkt. Gwajima amesema, tayari Tanzania imeandaa programu maalumu ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ambayo tayari imeonekana kufanya vizuri kimataifa na matokeo ya awamu ya kwanza yatapimwa mwaka 2026.

Mhe. Waziri Dkt. Gwajima amewasihi wadau wa mkutano huo na dunia kwa ujumla kuona umuhimu wa kuhakikisha ushiriki wa wanaume katika vita vya kupinga ukatili wa kijinsia unaoathiri sana wanawake na watoto huku akirejea uchache wa wanaume kwenye mkutano huo.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan, aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutano huo katika hotuba yake alikemea vikali vitendo vya ukatili kwa wanawake na kusema Ukatili kwa Wanawake ni Usaliti “Violence against Women is Betrayal”.

Mkutano huo ulioandaliwa na Serikali ya Uturuki kupitia Wizara ya Familia na Huduma za Kijamii ikishirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Wanawake na Demokrasia (KADEM) ulihudhuriwa na Mawaziri toka nchi mbalimbali duniani

Waziri Mhe. Dkt. Gwajima ametumia fursa hiyo pia kufanya mikutano ya Pembeni na Mawaziri wa Nchi za Algeria na Libya na kujadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kufanikisha maendeleo ya wanawake jambo ambalo litaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Tanzania, Aidha, Waziri Dkt. Gwajima katika mazungumzo na Waziri wa Wizara ya Familia na Huduma za Kijamii nchini Uturuki Mhe. Derya Yanik, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano.