November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanufaika Mpango wa TASAF
wapata mkopo asilimia 100

Na Mwandishi Wetu, TimesMajiraonline,Kilolo

WANAFUNZI wanne kutoka familia za Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya Kilolo, mkoani Iringa waliodahiliwa na vyuo vikuu kwa mwaka wa masomo 2022/2023 wamepata mikopo kwa asilimia 100 kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB)

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilolo, Lain Kamendu, wakati akizungumza na waandishi wa habari juzi, wilaya hapa kuhusiana mafanikio ambayo yanatokana na Mpango wa TASAF kuhudumia kaya hizo.

Amesema kaya za wanafunzi hao zilikuwa zikihuhudumiwa na TASAF tangu wakiwa elimu ya msingi, wakafaulu wakajiunga na O-Level na baada ya hapo wakafaulu tena wakaenda A-Level na kufaulu kujiunga vyuo vikuu na tayari wameishapitisha fomu zao za kuthibitishwa kwamba hao ni wale watoto wanaotakiwa kupata mkopo kwa asilimia 100.

Kamendu amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa fedha hizo kusaidia kaya maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, kwani kupitia fedha hizo wananchi wengi wamenufaika.

Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilolo, Lain Kamendu

“Kwanza kaya hizo za walengwa zilikuwa zinaishi maisha magumu sana, lakini kwa sasa zimepata unafuu kwa sababu kupitia fedha hizo zimeweza kuwa na miradi midogo midogo ambayo imewasaidia kwenye mambo mengi, ikiwemo kusomesha watoto. ” amesema.

Amesema miradi hiyo imewasaidia kupata uhakika wa chakula ambacho walikuwa hawawezi kupata kwa kukosa uwezo wa kuzalisha.

“Lakini wameweza kuwa na miradi midogo ya kuku, nguruwe, ng’ombe, mbuzi na wanajihusisha na kilimo. Miradi hii imewapa unafuu mkubwa, inawasaidia kusomesha watoto wao hadi wengine wamefainikiwa kudahiliwa vyuo vikuu na kujenga nyuma imara,” amesema na kuongeza;

Leo Kilolo, sio Kilolo iliyokuwa kabla ya Mpango wa TASAF kuanza. Mpango umekuwa na faida kubwa, haukuwasaidia tu kwa kupata chakula na kupata makazi, umeweza kusaidia hata watoto kupata elimu ambao watakuwa viongozi wa kesho, vinginevyo wangeishia mitaani.”

Amesema kwa maoni yake anashauri Mpango huo uendelee ili uweze kuendelea kusaidia wengi, kwani hadi sasa katika halmashari hiyo unahudumia kaya 9,499 zilizopo vijiji 110.

Hatua ya HESLB kutoa mikopo kwa asilimia 100 ni matokeo ya makubaliano baina yake na TASAF, ambapo wanafunzi wote wanaojiunga na vyuo vikuu kutoka kwenye kaya zinazohudumiwa na TASAF wanapata mkopo kwa asilimia 100.

Kinachotakiwa ni kuwepo barua ya uthibitisho kutoka TASAF, ambayo inaonesha namba ya mpango ya kaya husika na kwa kuwa imekubaliana na Bodi, HESLB imepewa namba ya kuiwezesha kuingia kwenye mfumo wa TASAF.

HESLB ikiingiza namba hiyo kwenye mfumo inaleta watoto wote wa kaya hiyo husika, hivyo kujiridhisha kuwa mtoto huyo anatoka kwenye kaya inayohudumiwa na TASAF hivyo kupatiwa mkopo kwa asilimia 100.

Kupitia makubaliano hayo, Kamendu alisema watoto wote kupitia mpango wa TASAF wakifika ofisi ya Halmashauri Kilolo wanapata uthibitisho na kujaza nyaraka zinazotakiwa kwenye mfumo wa HESLB, hivyo kuweza kupata mkopo asilimia 100 bila kikwazo.