Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Kilindi
CHUO cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga kitaanza kupokea wanafunzi kwa ajili ya masomo Januari, 2023 huku kikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,300 kwa ajili ya fani mbalimbali.
Fani hizo ni pamoja na ubunifu na ushonaji nguo, uhazili na kompyuta, ujenzi wa majumba, umeme wa majumbani, ufundi magari, na
fani ya Uchomeleaji na uungaji vyuma.
Hayo yalisemwa Oktoba 29, 2022 na Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Dakawa mkoani Morogoro Godfrey Kimwaga kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba ambaye alifika chuoni hapo kukagua ujenzi wake.
Kimwaga ambaye chuo chake cha VETA Dakawa ndiyo kimepewa jukumu la kusimamia na kuratibu ujenzi wa Chuo cha VETA Kilindi, alisema ujenzi wa chuo hicho unajumuisha ujenzi wa majengo 17, na ujenzi wake umefikia asilimia 97.
“Chuo hiki kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 300 wa kozi za muda mrefu na wengine zaidi ya 1,000 kwa kozi za muda mfupi. Chuo kinategemea kuanza kutoa mafunzo Januari 2023 kwa fani ya ubunifu na ushonaji nguo, fani ya uhazili na kompyuta, fani ya ujenzi wa majumba, fani ya umeme wa majumbani, fani ya ufundi magari, na fani ya uchomeleaji na uungaji vyuma.”
“Ujenzi huu unajumuisha ujenzi wa majengo 17 ikiwemo karakana ya ushonaji, karakana ya kompyuta na uhazili, kakarana ya ufundi wa magari na uchomeleaji vyuma, karakana ya umeme na uashi, jengo la utawala (Administration Block), madarasa mawili ya masomo mtambuka na Ofisi (General class room), bwalo la chakula na jiko, nyumba ya mkuu wa chuo, bweni la wasichana, bweni la wavulana, stoo, jengo la jenereta, vyoo vya watumishi, vyoo vya wanafunzi wavulana, na kibanda cha ulinzi” alisema Kimwaga.
Kimwaga alisema, mradi wote umekadiriwa kutumia sh. 2,446,591,559 hadi utakapokamilika. Hadi sasa fedha zimetolewa katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni sh. bilioni 1.6, na awamu ya pili ni sh. 846,591,557, huku fedha zilizotumika zikiwa sh.
2,446,591,559.
Kimwaga alieleza changamoto zilizojitokeza kipindi cha utekelezaji wa ujenzi wa chuo hicho ambazo zimesababisha kuchelewesha mradi kukamilika ndani ya muda uliopangwa ikiwemo miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki kwa usafirishaji wa malighafi za ujenzi haswa kwa kipindi hiki barabara ilivyoharibiwa na mvua.
“Wasafirishaji wengi hawakubali kusafirisha malighafi za ujenzi kufika eneo la ujenzi, hata wachache wanao kubali kusafirisha gharama inakuwa zaidi ya ile ya awali. Lakini pia kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi, hivyo bei kutoendana na bei za kwenye BOQ.
Upatikanaji wa mzabuni wa kuweka aluminum aliyepatikana awali aliomba kujitoa kutokana na malighafi kutopatikana sokoni.
“Upatikanaji wa mbao za mninga eneo la ujenzi, tulilazimika kupata mzabuni mkoani Tabora. upatikanaji wa mafundi wenye sifa katika eneo la utekelezaji wa mradi imekuwa ni changamoto.
Eneo la mradi kuwa na miteremko mikali pamoja na miamba, na kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi hivyo bei kutoendana na bei za kwenye BOQ” alisema Kimwaga.
Alisema ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa asilimia 100, wanahitaji sh. milioni 322 kwa ajili ya kazi kama kuweka aluminium, milango, terrazzo na kufunga taa kwa baadhi ya majengo ambayo hayajakamilika kutokana na changamoto hiyo ya fedha.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kumaliza ziara ya siku mbili wilayani Kilindi, Mgumba alisema ameridhika na miradi inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo, kwani pamoja na Serikali kutoa fedha, bado wananchi wameonesha ushirikiano katika kupokea miradi hiyo.
“Nimeridhishwa na ujenzi unaondelea kwenye miradi mingi ya Wilaya ya Kilindi hasa namna wananchi wanavyochangia utekelezaji wa miradi. Nimeona kuna miradi ya maji, afya na elimu inaendelea maeneo mbalimbali. Chuo cha VETA Kilindi ni mkombozi kwa Wanakilindi kwa watoto wao kusoma na kujipatia ajira kwa kujiajiri wenyewe ama kuajiriwa.
“Wito wangu, tutekeleze miradi kwa Sera, miongozo na maagizo yetu. Nawapongeza wananchi wa Kata ya Kimbe kujenga vyumba vinne (4) vya madarasa kwa gharama zao wenyewe, kama Serikali ingejenga, zingetumika sh. milioni 80, na ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan, kama Mama, amewapa sh. milioni mbili. Pia niwapongeze Kata ya Bokwa kujenga madarasa sita kwa sh. milioni 60. Madarasa matatu mapya samani zake, na matatu ya kumalizia ujenzi. Ubora wa majengo Hospitali ya Wilaya ni mzuri, ila sijaridhishwa sababu mradi umechelewa” alisema Mgumba.
More Stories
Wafanyabiashara wakutana Dar,kujadili hali ya biashara
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo