Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Mripuko wa Maradhi ya Surua ni tatizo la Ulimwengu wote, bali kinachohitajika ni taarifa sahihi, uelewa, na tahadhari kwa kila upande.
Othman ameyasema hayo jana akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Afya ya Zanzibar, huko Vuga Mjini Unguja, baada ya kukamilisha Ziara yake Maalum katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Jijini hapa, akikagua Maendeleo ya Juhudi za Kukabiliana na Tatizo la Surua lililoibuka kwa kasi, hivi karibuni, ndani na nje ya Nchi.
Amesema kuwa kimantiki kasi ya maambukizo ya Surua hapa Visiwani inaonekana ni kubwa, kwa kuzingatia uhaba wa raslimali na maandalizi duni ya kukabiliana na janga hilo, bali si vyema kukuza taarifa za uwepo wa maradhi hayo, kwa nia ya kuwatishia wageni na wale wanaopanga kutembelea Zanzibar.
“Maambukizo haya siyo suala la Zanzibar na Wala Wizara ya Afya pekee bali ni la ulimwengu mzima na linahitaji hima na juhudi za kila mmoja wetu ili kuweza kukabiliana nalo”, amesema Othman.
Hivyo amesema kuwa kwa sasa kunahitajika misaada ya hali na mali, sambamba na juhudi za pamoja ili kukabiliana na janga hilo, ambapo kila mmoja anawajibika kusaidia kwamujibu wa uwezo na nafasi yake.
Aidha, Othman amesisitiza umuhimu wa kujenga uelewa kwa wananchi na jamii kwa ujumla, juu ya maambukizo hayo kwa kutumia mbinu mbali mbali, zikiwemo njia sa sasa za mawasiliano, huku akipongeza juhudi zinazochukuliwa na waganga na wauguzi wa Hospitali hiyo, katika kukabiliana na Mripuko wa Maradhi ya Surua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dokta Salim Nassir Slim, ameshukuru hatua za Serikali ya Zanzibar, ikiwemo Ziara ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, kutembelea na kuhamasisha juhudi za Madaktari kupambana na Maradhi hayo.
Akigusia juu ya mtawanyiko wa kuenea kwa maradhi hayo hapa Visiwani, Dokta Slim amezitaja Wilaya za Magharibi A na B Unguja, kutokana na sababu mbali mbali, zikiwemo za kijeografia na uwezo wa kipato miongoni mwa wananchi na wakaazi wake, huku akibainisha Mkakati wa Kampeni ya Nyumba-kwa-Nyumba, kwaajili ya kuwapatia Chanjo, Watoto chini ya Umri wa Miaka 5, ifikapo Disemba 10, Mwaka huu.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Bi Zubeida Mohamed Hussein, ameeleza uzito wa kukabiliana na Mripuko wa Maradhi hayo Hospitalini hapo, na zaidi kutokana na uhaba wa nyenzo, uchache wa Vitanda vya Kulaza Wagonjwa, na uelewa duni wa mazingira ya maambukizi yake, ndani na nje ya wodi.
Kwa mujibu wa Takwimu za Wizara hiyo, takriban Watu 1315 wamepata maambukizo ya Ugonjwa huo wa Surua unaotibika na ambao unaambukizwa na Virusi, tangu uliporipuka hapa Visiwani mnamo Julai Mwaka huu; 997 kutoka Unguja, na 318 kisiwani Pemba, huku Watoto wapatao 8 wakiwa tayari wamefariki.
Ziara hiyo imeongozwa na Waziri wa Afya wa Zanzibar na Naibu wake Nassor Ahmed Mazrui na Hassan Khamis Hafidh; Wakurugenzi, Watendaji na Baadhi ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato