November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini Mbeya wajengewa uelewa bima ya afya kwa wote

Na Esther Macha,Timesmajira Online, Mbeya

VIONGOZI wa dini mkoani Mbeya wameipongeza serikali kwa kuja na mpango mahususi wa kusaidia jamii kwa kuleta muswada pendekezwa wa wa sheria ya Bima ya afya kwa wote kwani sio watanzania wote wana uwezo wa kiuchumi wa kuwawezesha kupata matibabu .

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa kamati tendaji ya CCT mkoa wa Mbeya Padri. Daudi Sichinga wakati wa mafunzo ya kujengewa uelewa kuhusu muswada pendekezwa wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote yaliyofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.

Padri Sichinga amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chgini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya jambo la msingi sana hasa ukizingatiwa sio watanzania wote ambao wana uchumi ambao utawawezesha kupata matibabu .

“Mswada huu pendekezwa wa sheria ya Bima ya afya kwa wote itasaidia wananchi wengi kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua hivyo bima hii ya afya kwa wote imekuja muda mwafaka tunaamini sisi viongozi wa dini tunaenda sasa kuelimisha waumini wetu ili waone umuhimu wa jambo hili kwao na tunaamini wengi wao watalipokea”amesema.

Kwa upande wake Sheikh Ibrahim Bombo, alipongeza Wizara ya afya kupitia uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa kuona umuhimu wa kuwajengea uelewa viongozi wa Dini na kusema katika Dini swala la Amani, Chakula na Afya ni muhimu kwa kuwa waumini ili waweze kupata maagizo ya Mwenyezi Mungu ni lazima wawe na afya njema.

Shekhe Bombo amesema suala la afya ni muhimu kwa kila mwananchi hivyo kama viongozi wa wadini watakikisha kila muumini elimu hiyo inamfikia kikamilifu .

Aidha, Mchungaji kutoka Jumuiya ya Makanisa kipentekoste Tanzania, Bi. Erika Mwakyolile amesema swala la Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ni kama Serikali ilichelewa sana, wao kama watumishi wa Mungu watashirikiana na Serikali bega kwa bega kuelimisha jamii kwa kuwa afya ni muhimu hivyo jamii kama vile inavyochangia sherehe nyingine, pia wachangie bima ya afya kwa kuwa ni muhimu kuliko sherehe kwa ustawi wa afya zao.

“Na nitoe rai kwa watu wote, hata kwa Serikali kwamba ni kweli tulichelewa sana na tunashukuru kwa muamko huu, sisi kama watumishi wa Mungu wa Dini mbalimbali ya Kiislam na Kikristo tunaamka kwa nguvu zote kwenda kuelimisha watu wetu” Mchungaji Erika Mwakyolile

Akizungumza katika mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji amewashukuru viongozi wa Dini wa mkoa wa Mbeya kwa umoja na ushirikiano waliouonyesha katika kuendelea kuitakia heri Hospitali.