November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makarani wa Sensa watakiwa kujaza madodoso kwa weledi katika zoezi la sensa 2022

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga.

Zikiwa zimesalia siku 22 kuelekea zoezi la sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 inayotarajiwa kufanyika Aguost 23 mwaka huu makarani, wasimamizi tehama na maudhui waliopo ndani ya mkoa wa Tanga wametakiwa kujaza madodoso kwa weledi na kuzingatia takwimu sahihi zitakazoisaidia serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo endelevu.

Rai hiyo ilitolewa na mratibu wa sensa mkoa wa Tanga Tony Mwanjota wakati alipotembelea mafunzo yanayolewa kwa makarani hao wakiwemo pia watendaji kata ndani ya halmashauri ya jiji la Tanga ambapo alisema kuwa kabla ya kufanyika kwa zoezi la kuhesabia watu utaanza ukusanyaji wa sensa ya majengo itakayofanyika kwa siku tatu ambapo ameitaka jamii kutoa ushirikiano kwa makarani hao.

“Mafunzo haya yanawasaidia makarani kwenda kukusanya takwimu ambazo zitatakiwa kujazwa madodoso ambayo yataonyesha taarifa sahihi zitakazosaidia katika mipango ya maendeleo ya nchi yetu , sensa hii tutaanza na sensa ya watu kwa siku sita baada ya hapo itafuata sensa ya majengo kwa siku tatu wito wangu kwa makarani wazingatie wanayofundishwa ili waweze kwenda kukusanya takwimu sahihi zitakazoisaidia kuleta maendeleo katika nchi yetu” alisema Mwanjota.

Awali akieleza namna walivyojipanga katika zoezi hilo mratibu wa sensa ndani ya jiji la Tanga Juma Mkombozi alisema kuwa jumla ya makarani 1448 wakiwemo wasimamizi wa maudhui na tehama pamoja na watendaji wa kata 27 wapo kwenye semina elekezi na tayari mafunzo yanaendelea yakitarajiwa kuchukua takribani siku 19 kabla ya kuelekea zoezi hilo la kitaifa litakalofanyika Augosti 23, 2022.

“Tayari tulishapokea vifaa kwaajili ya vifaa vya kufundisha kwa njia ya nadharia na vitendo na mafunzo yalianza vizuri na bado tunaendelea tutegemea ndani ya siku 19 na washiriki wote watafundishwa namna nzuri ya kwenda kuchukua taarifa kwenye kaya na maeneo mengine ikiwemo takwimu za majengo na huduma za jamii kwa ngazi za mitaa” alisema Mkombozi.

Aliwataka wananchi wote waliopo ndani ya halmashauri ya jiji la Tanga kuendelea kuelimishana na kuhamasika huku akiwataka kujipanga na kutoa taarifa sahihi kwa makarani ambazo zitaiwezesha serikali kutoa na kupanga huduma mbalimbali za kijamii kulingana na mahitaji ya maeneo husika.

“Hamasa mpaka Sasa tunaendelea nayo pamoja na kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari lengo ni kuhakikisha watu wote wanapata elimu na wanahamasika wananchi wote watoe ushirikiano kwa makarani na tuangalie zile taarifa muhimu zinazohitajika , ushiriki wa sensa ndio msingi wa ugawaji wa rasilimali za serikali katika kuleta maendeleo , tunachoamini mpaka ifikapo tarehe 23 kila mwananchi atakuwa tayari kujitokeza kuhesabiwa , ” alisema Mkombozi.

Kwa upande wake afisa mtendaji wa kata ya Pongwe Erika Njana alisema kuwa kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa wamejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anahamasika na kupata elimu sahihi ya Sensa ili aweze kujitokeza na kushiriki kikamilifu kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

“Sisi Kama viongozi wa kata tunalo jukumu kubwa sana kwa kushirikiana na kamati za kata kuhakikisha kuwa tunaendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kupitia zoezi hili la sensa bila kuwashirikisha viongozi hawa wa ngazi za chini itakuwa ni ngumu , sensa ni zoezi muhimu kwani bila sensa sisi kama wananchi hatuwezi kuona maendeleo” alisema Njana.

Mafunzo hayo ambayo yalianza July 31 yatahitimishwa augost 20 mwaka huu kwa ngazi ya tatu inayozijumuisha halmashauri zote 11 za mkoa wa Tanga.