Na mwandishi wetu, Timesmajira online
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa kuna wajibu kwa Mamlaka kuzijengea hadhi Taasisi za Elimu ya Juu, kwani ni tegemeo la maendeleo katika nyanja zote za maisha kwa Bara zima la Afrika.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Julai 25, kupitia Hotuba yake iliyowasilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, katika Ufunguzi wa Kongamano la Siku Nne Juu ya Hadhi ya Elimu ya Juu kwa Vyuo Vikuu vya Afrika, linalofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo Kiembe samaki Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.
Amesema kuwa Vyuo Vikuu, kutokana na umuhimu wake mkubwa, vimeendelea kuwa chanzo kikuu cha maarifa, mafunzo ya kitaalamu na stadi muhimu za miongozo juu ya namna ya kuivusha Afrika yote, kuelekea katika hatua mbalimbali za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Dkt. Mwinyi amezieleza Taasisi za Elimu ya Juu Barani Afrika kwamba, pamoja na changamoto nyingi zinazokabiliana nazo, bado zimekuwa ni daraja muhimu la kuwaunganisha watu hasa wanataaluma, na hivyo kujengeana uwezo kupitia uzoefu na mbinu mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Dkt Mwinyi ametaja baadhi ya changamoto hizo, zinazodhoofisha hadhi na ubora wa elimu ya juu Barani Afrika, kuwa ni pamoja na ongezeko la udahili mbele ya miundombinu dhaifu; ufinyu wa bajeti na uchache wa raslimali; ugumu wa kufanikisha tafiti na uhaba wa vitendea-kazi, hali ambayo inaathiri moja kwa moja ufanisi katika ufundishaji na hivyo kutokwenda sambamba na hali ya mabadiliko, katika ulimwengu wa sasa unaohitaji wahitimu bora.
“Mtakubaliana nami kwamba Vyuo Vikuu pamoja na Taasisi za Elimu ya Juu zinabaki kuwa na umuhimu wa pekee na chanzo kikubwa cha ujuzi wa kitaalamu, muhimu sana kwa nyanja zote za kimaisha na katika kukabiliana na changamoto au vikwazo vinavyozorotesha maendeleo ya Bara la Afrika”, ameeleza Mheshimiwa Dokta Mwinyi.
Ameongeza kuwa taatisi hizo ni chechem za kufunza na kuendeleza nguvukazi kwaajili ya viwanda, asasi mbali mbali, taasisi za Serikali, na kwamba kunahitajika mipango na mikakati imara itakayoijengea hadhi na ubora sekta hiyo muhimu, ili pia kukuza ufanisi kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa na Afrika kwa ujumla.
“Kwa hivyo, Afrika sasa inahubiri mapinduzi ya kiuchumi kwa sekta mbali mbali, hadhi na ubora wa elimu ya juu bila shaka ni mambo yanayohitajika mno ili pia kuweza kufikia malengo”, amesisitiza Mheshimiwa Dk. Mwinyi.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Ali Abdulghulam Hussein, amepongeza juhudi za kuasisiwa kwa umoja huo, akisema kuwa hiyo ni hatua muhimu itakayoweka dira ya kukuza hadhi ya Elimu ya Juu ndani ya Bara la Afrika.
Naye, Mratibu wa Kongamano hilo, Dr. Violet Makuku kutoka nchini Ghana, amezihamasisha taasisi za elimu ya juu katika Mataifa mbali mbali, kufanya hima kujiunga na Umoja wa Vyuo Vikuu Afrika, ili kunufaika na fursa nyingi ziliomo, zikiwemo nafasi za ajira kwaajili ya wasomi, wahitimu na wataalamu, na kwa maendeleo ya Bara zima.
Waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Maafisa Wakuza Hadhi, Viwango, Mitandao na baadhi ya Wasaidizi Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Afrika, Wakiwemo kutoka Nchi za Kenya, Uganda, Somalia, Misri, Malawi, Burundi, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Nigeria, Lesotho, Eswatini, Botswana, Namibia, Afrika ya Kusini, na wenyeji Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Viongozi mbali mbali wa Serikali, aidha wamejumuika katika Kongamano hilo la Siku Nne, wakiwemo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Profesa Mohamed Makame Haji; Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dr. Omar Dadi Shajak; na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika, Profesa Olusola Bandele Oyewole.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu