November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yatoa vifaa vya Afya na Elimu Wilaya ya Lushoto

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB imetoa msaada wa mabati 200 kwa Zahanati ya Kwemakame iliyopo wilayani Lushoto mkoani Tanga yenye thamani ya Sh. milioni 7.1 na madawati 50 katika Shule ya Msingi Mbula B iliyopo wilayani humo yenye thamani ya Sh.milioni 3.9 ambapo jumla ya msaada huo ni Sh. milioni 11.

Awali akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper alisema kuwa benki hiyo inatambua juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan za kusimamia huduma za afya na elimu kwa nguvu zote kwa kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma hizo mjini na vijijini.

Meneja huyo wa kanda alisema walipopata maombi ya kuchangia katika maendeleo ya elimu kwa Wilaya ya Lushoto walifarijika na kushirikiana nao ili ikawe chachu ya maendeleo ya sekta ya afya na elimu kwa jamii yao hasa katika zahanati ya Kwemakame na kwa Shule ya Msingi Mbula B.

Aliongeza kuwa imani yao ni kuwa vifaa hivyo vitatumika vyema kwa manufaa makubwa ya wananchi wa wilaya hiyo. ” Vifaa vinavyokwenda shuleni basi watoto wetu na wadogo zetu watakwenda kunufaika vyema kabisa na hata kusaidia ufaulu wao.,” alisema na kuongeza:

“Benki ya NMB tumekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu kwa jamii, ni kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tumekuwa tukitenga asilimia 1% ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka, “alibainisha Prosper.

Awali akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalist Lazaro aliishukuru benki hiyo kwa msaada huo na kueleza kuwa msaada huo wa madawati unakwenda kuwatoa watoto wao kwenye vumbi na hatimaye sasa kukaa kwenye madawati huku mabati hayo yakienda kusaidia kwenye huduma za afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Ikupa Mwasioge alisema benki hiyo imekuwa ikijihusisha na utoaji wa misaada katika jamii zao kwani mbali na msaada huo hivi karibuni waliwapatia msaada wa vifaa katika kituo cha afya cha Mlalo.

Mjumbe wa kamati ya shule hiyo alisema kwa niaba ya kamati ya shule na wazazi wa kijiji hicho wameishukuru benki ya NMB kwa kuwapatia msaada huo ambao unakwenda kuongeza ufaulu shuleni hapo.

“Haya mabati 200 yanakwenda kutusaidia katika Zahanati yetu ya Kwemakame kuezeka kwani ilijengwa na bado haijaezekwa mabati, “alisema William Aloyce – Mtendaji wa Kijiji cha Kwemakame Kata ya Kwai.

Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini(wa nne kulia), Dismas Prosper akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalist Lazaro(kulia) mabati 200 yatakayokwenda kutumika katika Zahanati ya Kwemakame iliyopo Wilayani humo.
Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper akimkabidhi madawati 50 Mkuu wa wilaya ya Lushoto Kalist Lazaro kwajili ya shule ya Msingi Mbula B iliyopo Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga.