November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji wa sekta ya mifugo na maji wapewa saa 24 kutatua changamoto ya usimamizi wa mifugo

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Serikali mkoani Tanga imetoa saa 24 kwa watendaji wa sekta ya mifugo na maji kuhakikisha wanatatua changamoto ya usimamizi wa mifugo ya wananchi waliohamia mkoani humo katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni, kutoka katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Hatua hiyo imekuja siku chache tangu wananchi hao kuhamia kijijini hapo na mifugo yao ambapo jana Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima alikutana wananchi hao na watendaji ili kusikiliza changamoto zao ambapo changamoto tatu ziliibuliwa ikiwamo utambuzi wa njia za kupitisha mifugo, mabwawa ya maji, maeneo ya malisho na josho.

Kutokana na hatua hiyo, Malima alitoa agizo hilo la saa 24 kwa watendaji huku akisisitiza kesho yawe yametekelezwa ili wananchi hao waendelee na maisha yao kama walivyokuwa wakiishi Ngorongoro.

Malima alisema yuko tayari kuhamia kijijini hapo kuhakikisha wananchi hao wanapata huduma stahiki kama walivyokubalina serikali na watendaji kabla wananchi hao hawajahamia kijiji hapo.
“Nataka ninapoondoka hapa leo, kesho nikiruidi hapa tuondokane na changamoto hizi. Inawezekana kwenye mfumo wote tulioweka hatujatimiza au hatujafanikiwa kwa yale yote kama tulivyotaka lakini yako mambo ya msingi ambayo tulikubaliana, tulisema mifugo ikija lazima ipate sehemu ya maji,” alisema Malima.

Aidha, Malima aliwataka watendaji hao kutumia muda wa siku moja kukamilisha shughuli hiyo ya kuwapatia na kuwaonyesha wananchi hao sehemu ya kulishia mifugo, sehemu za malisho watakazokwenda, bwawa la maji kuwanyweshea huku akisisitiza hataki kusikia mambo mengine tofauti.

“Hakuna kero kuna changamoto, na ukweli ni kwamba watazoea kama sisi tulivyozoea kwa sababu tunajua kabisa wakati tunasubiri kupokea ugeni huu wote tumejitahidi hakuna idara ambayo haijajjitahidi kutimiza wajibu wake.

“Na ndiyo maana nasema mimi nitahamia huku na ikiwezekana katika zile nyumba moja nitachukua mimi nitakaa hapa mpaka kitaelekeweka. Kwa hiyo hayo yote matatu nataka yakamilike leo yaani kesho tuondokana na changamoto hizo.

“Nataka mambo hayo matatu yawe yamekamilika wageni wangu hawa wawe wamejua maeneo hayo waliyoainisha wajue kabisa kwamba ng’ombe zao zinapita hapa siyo huu mpango wenu wa A, B, C, D… hawauelewi hata miomi siuelewi,” alisema.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa agizo hilo kwa upande wa sekta ya maji, Meneja wa Wakala wa Maji, Mjini na Vijijini (Ruwasa), Wilaya ya Handeni, Joseph Mungizi alisema kuna eneo ambalo walishaonyeshwa ambalo ndiyo walikuwa wananyweshea mifugo na walishaanza zoezi la kuchimba mashimo ambayo ng’ombe wataendelea kupata huduma pale wakati wanaendelea na ujenzi wa mbauti.

“Kwa hiyo ni jambo ambalo tumelichukua na tutaongeza kasi katika kulitatua. Lakini kingine ambacho tumefikiria kukifanya kwa sababu pale pale wanaponyweshea mifugo kuna kisima cha zamani ambacho kina maji mengi tu, ingawa yana chumvi lakini ng’ombe wanaweza kutumia kwa hiyo tutaongea na wenzetu wa Tanesco watusaidie tuweke mbauti nadhani hiyo itakuwa suluhisho la kudumu.

Kwa upande wake Afisa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Alfred Mushi alisema kesho (leo) watatekeleza agizo hilo la mkuu wa mkoa kwa kuwaonyesha wafugaji njia za mifugo kuelekea kwenye maeneo ya malisho kwa sababu maeneo yako tayari yameshainishwa, yana malisho mazuri na maji yapo ya kutosha.

“Suala la mojosho tayari yameshakamilika na uogeshaji wa mifugo utaanza kesho rasmi na tayari tumeshaweka maji, dawa tutaziweka kesho asubuhi. Majosho matatu tayari yameshakamilika, kuna majosho manne tunatengeneza tena mengine na mkandarasi ameshaingia site anaanza kazi,” alisema.