November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahisa Benki ya NMB waidhinisha gawio Bil. 96.7/-

Wanahisa wa Benki ya NMB wameidhinisha gawio la Sh 96.7 bilioni kwa mwaka 2021, huku wakiwa na imani
kubwa benki yao kuendelea kufanya vizuri zaidi mwaka huu.
Gawio la mwaka 2021 linatokana na kuongezeka kwa faida baada ya kodi kutoka Sh206 bilioni mwaka 2020 na
kufikia Sh290 bilioni mwaka jana, mwaka 2021.
 
Katika Mkutano wake Mkuu wa 22 wa Mwaka uliofanyika mwishoni mwa wiki, wanahisa walipitisha kiasi hicho cha
fedha ambacho ni sawa na malipo ya Sh193 kwa kila hisa kwa kipindi kilichoishia Desemba 31, 2021 (wanahisa
walipata gawio la Shs 137 kwa kila hisa kwa mwaka 2020).
 
Akizungumza na wandishi wa habari, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB- Ruth Zaipuna alisema Benki hiyo
itaendeleza mwenendo wake wa kufanya vizuri kwa kuvuka malengo iliyojiwekea kwa mwaka huu pia.
 
Matarajio hayo yanatokana na matokeo mazuri ya robo ya kwanza ya mwaka huu ambapo Benki tayari imepata
faida baada ya kodi ya Sh101bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 55 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka
jana.
 
“Ni kweli tumeuanza mwaka 2022 vizuri. Mafanikio makubwa ya kiutendaji kwa mwaka 2021 na matokeo mazuri
ya robo ya kwanza ya mwaka 2022 ni kielelezo cha ufanisi mzuri unaotokana na utekelezaji makini wa mikakati
yetu. Tutaendelea kutekeleza kwa umakini sana mikakati tuliyojiwekea na tunaamini kwamba malengo
tuliyojiwekea kama benki tutayafikia na kuyapita mwaka huu wa 2022,” alisema Zaipuna.
 
Alisema kwa mahesabu ya kawaida, matokeo ya robo ya kwanza ya mwaka huu yanaleta picha kuwa utakuwa
mwaka mzuri pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza duniani. “Kadri tunavyoendelea kukabiliana na
mazingira ya biashara yanayobadilika kwa kiasi kikubwa, tumejipanga kwa umakini kupata matokeo mengine
mazuri yatakayoendeleza rekodi yetu sokoni” alisema.
 
Mwaka jana, Benki ya NMB ilifanikiwa kuvuka malengo yake katika vigezo karibu vyote vya kiutendaji, huku amana
za wateja zikipanda hadi Sh6.6 trilioni na mikopo ikifikia Sh4.8 trilioni.
  
Benki hiyo pia imeweka rekodi katika sekta ya benki kwa kuwa na uwiano bora wa gharama za mapato wa asilimia
46 hadi kufika Desemba 31, 2021 ikiwa imepungua kwa asilimia 5 ikilinganishwa na mwaka 2020 (asilimia 51), huku
uwiano wa mikopo chechefu (NPL) ukifikia asilimia 4 ya mikopo ghafi, kiwango ambacho ni chini ya kile
kinachotakiwa na Mdhibiti (Benki Kuu).

Kwa ujumla katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita benki ya NMB ilishuhudia Mizania bora, ukwasi wa kutosha
na viwango thabiti vya mtaji ambavyo viko juu ya viwango vya udhibiti. Benki hiyo pia ilitambulika kimataifa kama
benki bora na salama.
 
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede alisema “Tumeendelea kudhihirisha ufanisi na
ustahimilivu mkubwa kwenye biashara. Tutaendelea kujumuisha mafanikio makubwa yaliyopatikana, tuendelee
kuzingatia kuwainua wafanyakazi wenye ujuzi unaofaa ili kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi. Ninawahakikishia
wanahisa wote wa Benki ya NMB, dhamira ya Bodi ni kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuongeza faida kwa
wanahisa wetu kwa miaka mingi ijayo”.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akimkabithi Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB,
Dk. Edwin Mhede ripoti ya mwaka 2021 kwenye Mkutano Mkuu wa 22 wa Wanahisa, uliofanyika ukumbi wa
JNICC, Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori na Kaimu katibu wa NMB,
Consolatha Mosha.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 22 wa
Wanahisa, uliofanyika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam.