November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ARU yabuni teknolojia ya ujenzi rafiki kwa mazingira

Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraonline,Dodoma

Chuo Kikuu Ardhi (ARU), kupitia Taasisi yake ya Utafiti ya Nyumba wamebuni teknolojia ya ujenzi wa gharama nafuu kwa kutumia matofali ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Hayo yalibainika wakati wa maonesho ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayoendelea kwenye viwanja vya kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.

Akizungumza kuhusu teknologia hiyo, Mhadhiri wa ARU Dkt. Given Mhina amesema matumzi ya tofali za aina hiyo zitasaidia kupunguza hewa ya ukaa duniani, kutunza na kuhifadhi mazingira.

Mhandisi wa Ujenzi wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Twimanye John, akionyesha teknolojia rahisi ya kutengeneza tofali ambazo ni rafiki kwa mazingira kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center mkoani Dodoma

Amesema tofali hizo hutengenezwa kwa kutumia udongo wa mfinyanzi, saruji na maji kidogo .Tofali hizo ni imara kwa matumizi mbalimbali ya shughuli za ujenzi.

“Tumekuja na teknojia hii kama sehemu ya jitihada ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa unaotokana na shughuli za ujenzi na mali ghafi zake kama vile saruji, mchanga na maji…. tunatumia udongo wa mfinyanzi na wakati mwingine vumbi linalotokana na utengenezaji wa kokoto,” amesema

Amesema ujenzi wa nyumba kwa kutumia tofali hizo hauhitaji saruji, mchanga wala maji kwani zinafungamana zenyewe isipokuwa wakati wa kuweka nguzo za nyumba pekee.

Mhandisi wa Ujenzi wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Twimanye John, akielezea teknolojia rahisi ya kutengeneza tofali ambazo ni rafiki kwa mazingira kwa wageni waliofika kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center mkoani Dodoma

Dkt. Mhina amesema hata wakati wa umaliziaji wa nyumba mtu aliyetumia tofali hizo halazimiki plasta ya saruji na mchanga badala yake mafundi watatumia mchanga na saruji kidogo sana kuziba mashimo na kisha mwonekano wa nyumba kuwa wa kuvutia.

Mtaalamu huyo amesema faida nyingine ya matumizi ya matofali ya aina hiyo ni kutosababisha joto ndani ya nyumba kulinganisha na matofali mengine yaliyozoeleka kwenye shughuli za ujenzi.

“Tofali zinazotengenezwa kwa kutumia saruji na mchanga zinatabia ya kufyonza joto wakati wa mchana na joto hilo kutoka wakati wa usiku lakini mfinyanzi unaotumika kutengeneza tofali hizi unasababisha ubaridi kwasababu hauna tabia ya kufyonza joto,” amesema

Mhandisi wa Ujenzi wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Twimanye John, akielezea teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na Taasisi ya Utafiti wa Nyumba ya ARU kwa wageni waliofika kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center mkoani Dodoma

“Ndiyo sababu kwenye chungu kilichotengenezwa kwa mfinyanzi ukiweka maji hata mchana wakati wa joto kali baada ya muda maji yanapata ubaridi na watu wengi wamekuwa wakitumia vyungu vya mfinyanzi kupata maji baridi,” amesema

Dk. Mhina amemalizia kwa kusema kuwa Taasisi ya Utafiti wa Nyumba ya ARU imekuwa ikifanya tafiti kwa vifaa vya ujenzi vinavyopatikana hapa nchini na kwingineko duniani.

Ameseama jukumu lingine la taasisi hiyo ni kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazofanya zinawafikia walengwa kukuza na kuendeleza matumizi ya vifaa bora vya unjenzi nchini.