Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani na wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa imeweka mkakati wa kuongeza kasi ya uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19 nchini kupitia kampeni iitwayo Global VAX Initiatives yenye lengo la kuchanja wananchi 59,000 kwa siku.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Global Vax Initiatives uliofanyika katika viwanja vya Mwembeyanga Temeke jijini Dar Es Salaam.
Waziri Ummy amesema uzoefu uliopatikana katika awamu mbili za utekelezaji wa kampeni umeonyesha kuwa kasi ya matumizi ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 huongezeka zaidi wakati wa kampeni na mwenendo wa hali ya uchanjaji hushuka baada ya kampeni na kupelekea Mikoa, Halmashauri na Vituo kutokufikia malengo ya kila siku yaliyowekwa.
“Tumebaini kuwa baadhi ya walengwa waliopata dozi ya kwanza ya chanjo zinazotolewa kwa dozi mbili hawajarudi kupata dozi ya pili. Mathalani, kwa kipindi cha mwezi Februari, 2022, wananchi ambao hawakurudi kupata dozi ya pili ya chanjo aina ya Sinopharm ni 308,164 (25%), chanjo aina ya Pfizer ni 147,345 (36%) na chanjo aina ya Moderna ni 161,580 (24%)”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameongeza kutokana na changamoto hizo kuna haja ya kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ili matumizi ya chanjo yawe endelevu. Ameongeza kuwa jitihada za kusogeza huduma ya chanjo kwa walengwa wapya zinatakiwa ziende sambamba na kufanya ufuatiliaji kwa waliopata dozi ya kwanza ili kutoa fursa kwa wao kupata dozi ya pili ya chanjo husika.
“Sambamba na kuzindua kampeni hii pia tunapeana maelekezo ya kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 nchini na kuhakikisha rasilimali fedha zinazotolewa na Serikali na Wadau zinaleta tija iliyokusudiwa nchini”. Amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameagiza Wadau Watekelezaji (Implementing Partners, IPs) wote wanatakiwa kushirikiana na Timu za Uendeshaji wa Huduma za Afya ngazi ya Mikoa na Halmashauri katika kuhakikisha afua za chanjo zinatekelezeka ikiwemo huduma mkoba na tembezi, Kuzifikia taasisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewahasa watanzania wote kupata chanjo ya UVIKO-19 lakini pia ametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya ulimwengu wa watu kuelewa umuhumu wa chanjo na kuruhusu chanjo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato